SOMO: KUSIKILIZA KWA BIDII – IBADA YA JUMAPILI EFATHA MINISTRY MWENGE

NENO NA MCHUNGAJI: AIMANA DOMINICK

Mch. Aimana Domonick

Kama hatutasikiliza kwa nia moja au kwa bidi sahau kupokea yale uliyo kusudiwa, lakini ili uweze kupokea cha kwako unapaswa kusikiliza kwa bidii.

Kuna jambo ambalo Mungu amekusudia wewe uweze kupokea ndani ya mwaka huu, lakini uwezo wa kupokea au kuto kupokea uko mikononi mwako. Ufanye nini ili uweze kupokea? Unapaswa kusikiliza kwa bidii Neno la Mungu ili kwamba uweze kupokea kile ambacho Mungu amekukusudia.

Matendo 8:4-8 “Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya……..”
Tunapo sikiliza NENO la Mungu kwa bidii tunaruhusu Roho Mtakatifu atupe kile kinacho zungumzwa.
Kwa nini inakuwa hivyo? Kwa sababu wakati mnenaji au Mhubiri anapokuwa anaongea habari ya magonjwa Roho wa uponyaji atakuwa akipita ili kuponya watu, na kama akiwa anaongea kuhusu habari ya ndoa, inakuwa ni sawa na anamruhusu Roho wa ndoa apite na kuponya ndoa zilizokuwa na shida na akiwa anaongea kuhusu maisha yetu au kazi za mikono yetu inakuwa ni sawa na anamruhusu Roho kupita na kuponya watu walio katika shida hiyo. Lakini katika yote haya unaweza kupokea kwa wewe kusikiliza kwa bidii, kwa maana kwa kufanya hivyo unamruhusu Roho Mtakatifu kufanya kazi yake na kukupa kile ambacho umekusudiwa kije kwako.

Sikiliza kwa Bidii Neno la Mungu ili uweze kukutana na muujiza wako.

Kunafaida unapo sikiliza kwa bidii.
1. Unamruhusu Roho Mtakatifu kufanyia kazi kile kilicho zungumzwa kwa haraka.
2. Mapepo yanapiga kelele na kutoka kwa watu, na kila nguvu iliyokuwa imemkandamiza mtu inaondoka.
Hayo yakitokea kunakuwa na furaha kubwa katika hilokusanyiko, lakini kama hatutakuwa na nia moja au kusikiliza kwa bidii yale maneno yatakayokuwa yakizungumzwa tutakuwa tunamzuia Roho Mtakatifu kufanya kazi yake.

Ili uweze kumuona Mungu akimruhusu Roho Mtakatifu kufanya maajabu ndani yako unapokuwa ibadani, ni lazima kwa nia moja umsikilize kwa bidii Mhubiri atakayekuwa akihubiri kwa maana kwa kufanya hivyo unampa nafasi Roho Mtakatifu kufanya kazi yake. Siku zote Roho Mtakatiu anapenda watu wenye nidhamu.

Kwa nini tunataka kumruhusu Roho Mtakatifu afanye hiyo? Kwa sababu uponyaji wa kiroho na kimwili ni sehemu ya injili, Neno la Mungu linapokuwa likihubiriwa na mtu akilisikiliza kwa bidii linaruhusu uponyaji wa kiroho na kimwili kutokea. Hivyo Uponyaji ni sehemu ya injili.

SOMO: KUTUMIWA NA MUNGU (MCHUNGAJI KIONGOZI MKOA WA ARUSHA – MCH: JAMES NYANSIKA)

Mch. James Nyansika

Lazima ujiulize Mungu anatumia watu kufanya nini? Wewe kama wewe unasababisha nini katika jamii? Umeokoka kwa muda mrefu una miaka 15 katika wokovu, unasababisha nini katika ufalme wa Mungu?
Kumtumikia Mung sio kuwa na magonjwa, Mungu hauwezi kumtumikia wakati ukiwa na magonjwa, maana fedha na nguvu zako zote utazipeleka kwenye magonjwa badala ya kupeleka katika kumtumikia Mungu.
Lazima uelewe kusudi ni nini?
Uwepo wetu wa kuwa hapa tunaona Amani tele, furaha inazidi kila iitwapo leo, tunatumaini la milele kwa sababu kuna mtu ambaye alikubali kutumiwa na Mungu. Je wewe kama wewe umefanya nini katika ufalme wa Mungu kwaajili ya Mungu?
Mtu anaye tumiwa na Mungu
• Anajenga madhabahu ya Bwana
• Anasikia Neno kutoka kwa Bwana.
• Ana utayari kwaajili ya Bwana.
• Wanaotumiwa na Mungu sio waoga.
Mungu anaangalia moyo wa yule aliye karibu naye. Unaomba maombi ili upate hela ili iwe nini? Unaomba Mungu akupe mke mzuri ili iwe nini? Lazima uwe na sababu kwaajili ya Bwana.

(1 Samweli 16: 7 “ Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi “) Lakini Bwana akamwambia Samweli,
Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.

Je Mungu akiutazama moyo wako anaona nini? Kuna watu kazi yao ni kusengenya na kuwasema watumishi wa Mungu, wanamaneno mengi, wanazungumza mengi, sasa unakuta wana maombi hata ya kuwaumiza wengine sasa jiulize wewe mwenyewe je unatumiwa na nani wewe, unasababisha nini kwa wengine ambao Mungu amekupa kuwa nao?
Je unasababisha Amani? Upendo ni nini? Maana Mungu anatazamam moyo, Lazima ujipange kutumiwa na Bwana, wale wote walioko tayari kutumiwa an Bwana hawana hofu ya kuogopa kupambana na shetani maana shetani mwenyewe anatimua mbio kwa sababu anakazi na Bwana.

Anayetumiwa na Bwana hatishiwi na kitu chochote. Je moyo wako una nini wewe? Maana Bwana anatazama moyo ili akutumie, saa Bwana anakuangalai moyoni mwako anaona nini? Wacha maombi yako yakawe kwaajili yaw engine na sio masengenyo ili shetani asipate nafasi.
Unaposema Mchungaji kanikwaza au hajanifurahisha unaacha kazi ya Mungu sikiliza unatumiwa na Mungu sio Mchungaji.
Amua kumtumikia Bwana utaona matunda yake.

Karibu katika Ibada zetu,

Kanisa la Efatha Ministry Arusha lipo Kimandolu

Kwa msaada/maombi wasiliana na Mchungaji No 0767 103 231

SOMO : NGUVU – MCHUNGAJI; DAVID ANDULILE MWAKISOLE.

Mch. Davide Mwakisole

Huu ni mwaka wa NGUVU, ukiona umeufikia mwaka huu wa NGUVU basi ujue kuwa unayo NGUVU ndani yako au kipo cha kukuvuta ili ufikie hiyo NGUVU.
Matendo 1:6-8” Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi”.

Wanafunzi wa Yesu walimuuliza Yesu kuwa wakati huu ndipo utakapowarudishia Israeli UFALME? Yesu akawajibu sio kazi yao kujua nyakati wala majira, yapo mambo ambayo ni ya Mungu mwenyewe sisi hatuna sababu ya kumuuliza kwa kuwa yapo kwenye mamlaka yake mwenyewe, na Yesu akawaambia lakini mtapokea NGUVU akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu nanyi mtakuwa MASHAHIDI wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. Kuna mambo mengine huwezi kupokea bila kuwa na Nguvu.

Roho Mtakatifu anapokuja kwa mtu anakuja na NGUVU kwa ajili ya kushuhudia, usipokuwa na NGUVU inamaana wewe ni DHAIFU na ukiwa DHAIFU huwezi kufanya chochote. Hata wanaotafuta wafanyakazi wanatafuta mtu ambaye sio dhaifu ili aweze kufanya kazi, hata maaskari hawachukuliwi watu dhaifu bali wenye NGUVU, udhaifu ni kukosa NGUVU unapokosa NGUVU mambo mengi yanakupita kwani unashindwa kufanya kazi, hivyo kataa kuwa dhaifu.

Ukiwa DHAIFU ni rahisi sana KUSHINDWA, Mungu aliyetuumba anatujua tuna NGUVU kiasi gani na tunaudhaifu kiasi gani, ndio maana akasema mtapokea NGUVU. NGUVU hii sio NGUVU ya kupigana bali ni NGUVU ya kushinda kile kinacho kutesa, NGUVU hii haionekani kwa macho ya kawaida na haiji kwa kula chakula kama ugali. NGUVU hii ni ile ambayo YESU alisema mtaipokea akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, anaposema mtapokea NGUVU inamaana ipo nguvu iliyo kinyume chako lakini ukiipokea hii NGUVU inayotoka kwa MUNGU itakupa kushinda ile nguvu ya yule adui.

NGUVU hii inagombana na vitu vilivyo ndani yako vinavyo sababisha ukifanya biashara haiendi, na chochote unachokifanya hakistawi. Yesu anasema mkisha kuipokea hiyo NGUVU mtakuwa MASHAHIDI wake kila mahali hivyo hakuna cha kukuzuia. Leo pokea NGUVU hii na ukawe MSHINDI.

Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Ukisha mwamini Bwana Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako Roho Mtakatifu anakuja kwako.
Pasipo imani huwezi kumpendeza Mungu ila ukiwa nayo utaweza kumpendeza Mungu naye ndipo atakupa nguvu ya kuweza kufanya yale ambayo yatampendeza YEYE.

Haya ni mambo ya kiimani unatakiwa kuyaangalia kiimani, hata dhambi haijaondoka duniani ila wewe umeokoka katika hao wenye dhambi, ndivyo ilivyo hata katika nguvu hii; kama ulishindwa mwaka jana usiangalie hayo amini kuwa mwaka huu utashinda.

Tumeingia mwaka wa nguvu ili kwamba tuweze kuwa washindi hivyo ili uweze kuwa mshindi amini ya kuwa umeshinda naye Mungu aliye Baba Yetu atakushindia.

UFANYEJE ILI UPOKEE HII NGUVU?

  1. Kama hujaokoka ni Lazima UMPOKEE BWANA YESU ili awae BWANA na MWOKOZI wa Maisha yako maana kwa kuokoka unafanyika mwana wa MUNGU naye MUNGU kupitia ROHO MTAKATIFU anakupa NGUVU. Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”
  2. KUMUAMINI Mtumishi wa MUNGU Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira aliyepewa UJUMBE huu kuwa mwaka 2018 ni mwaka wa NGUVU.
  3. Kusikiliza na kufanyia kazi kwa uaminifu masomo na maelekezo katika Ibada na maelekezo kutoka kwa Watumishi mbalimbali.

MUNGU AKUBARIKI SANA.

Kwa msaada Zaidi wasilina na Mchungaji kwa No 0754 753 182

HERI YA MWAKA MPYA 2018 – TANGAZO

TANGAZO LA MWAKA 2018

Isaya 40:29-31 “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; WATAPANDA JUU KWA MBAWA KAMA TAI; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”

Mwaka 2018 ni mwaka wa NGUVU , hutawahi kuzimia, hutawahi kushindwa hutawahi kuteswa, hutawahi kuwa dhaifu hutawahi kulala kwa sababu ya maradhi. NGUVU ya Mungu kutoka Mbinguni itakujia na kukutia NGUVU na kukupa kushinda.
Yale yote uliyoshindwa kufanya miaka iliyopita sasa utaenda kuyafanya kwa ushindi, ingawa unaonekana ni dhaifu lakini itatoka nguvu ndani yako na kushinda kila kizuizi kilichopo mbele yako, kamwe hutashindwa tena.

Mwaka huu utakwenda kufanya uharibifu katika kambi ya ibilisi, atalia ili kutafuta usaidizi na kamwe hataweza kupata, kilio na majonzi vitatawala katika kambi yake, popote utakapo tokeza kama kuna uchawi wowote kutakuwa na mpasuko na uharibifu mkubwa. Kama kuna mchawi au mganga wa kienyeji katika familia yako mwaka huu ni mwaka wa kuzika. Yeyote aliyekuwa anakuzuia kung’aa kamwe hataweza tena, mwaka huu ni mwaka wako kwa sababu ni mwaka wa NGUVU hivyo ushindi ni wako.

Watu wengi watatamani kukusogelea ili wainuliwe kwa sababu wewe utakuwa umeinuliwa, wakati wote kuanzia sasa hadi milele hutakuwa pekeyako kwa sababu utukufu wa Mungu utakuja katika maisha yako ili kusababisha NGUVU kuja kwako.
Kuhangaika na kung’ang’ania kumekwisha.

SOMO:KANISA NA UONGOZI WAKE – (Jumapili Desemba 16 / 2017)

MCHUNGAJI; BETSON KIKOTI:

Matendo ya Mitume 6:1-7 “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung’uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.  Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.

Hii ni historia ya Kanisa la kwanza, Bwana Yesu alipoanza kazi yake alionyesha kwamba kuna matumaini makubwa ya kuweza kuelekea ufalme wa Mungu. baada ya Yesu kuondoka ndipo Mitume walianza kazi na Roho Mtakatifu aliwaongoza. Petro siku yake ya kwanza kuhubiri alisababisha watu 3000 kuokoka, ilikuwa ni injili ambayo inaponya, asilimia kubwa ya watu walitamani kuifuata injili ya Yesu, na ndipo kila aina ya makabila yaliungana kumwendea Yesu.

Hii ndivyo ilivyo leo, tupo makabila mbalimbali kanisani sisi sote ni mali ya Yesu Kristo. Tukiwa pamoja tuna kazi ya kuweza kutengenezana kwa sababu sisi kila mmoja ametoka katika jamii aliyotoka na anatabia yake, hivyo ili kusiwe na manung’uniko tunahitaji kuweza kukaa na kutengenezana ili tuwe na tabia moja. Tunaona Kanisa la kwanza kulikuwa na ubaguzi wa kikabila kwani Wayahudi wa Kiyunani na Kiebrania walikuwa wana baguana, hivyo sisi kama kanisa hatupaswi kuwa na ubaguzi wa kabila ili kwamba tuweze kusababisha ufalme wa Mungu uweze kwenda mbele.

Viongozi wanapaswa kuwa makini na watu wanao waongoza ili kwamba kusije kukatokea mpasuko katika Kanisa.

Mahali popote watu wakiwa na manung’uniko vipawa vya Mungu vinaweza kuwa chini.

Kanisa linaweza kuwa na Heshima kama Viongozi wake wakiwa waaminifu, viongozi walio waaminifu wanaweza kusababisha kanisa linakuwa na Heshima.

Heshima aliyonayo kiongozi inaweza kusababisha watu wengi kuweza kusimama na kutaka kumjua Mungu zaidi.

Manung’uniko yanaweza kutokea kama ilivyotokea katika kanisa la kwanza, kwa sababu watu wanatoka katika jamii mbalimbali ambazo wamezoea kufanya jambo Fulani, kazi ya kanisa ni kuwaweka pamoja na kuwafanya wawe wamoja kwa kuwa na tabia moja.

Isaya 43:4 “Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.

Mtu yeyote aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anapendwa na Mungu nani wa thamani mbele zake, hivyo wewe ni wathamani na umeheshimiwa, usijidharau.

Mtu yeyote anaye kudharau usimuangalie huyo, inawezekana katika uongozi wako, kila wakati unaona kudharauliwa, Mungu anasema kuwa wewe ni wathamani na “kabla hujaingia tumboni mwa mama yako alikujua na kabla hujatoka alikutakasa”, wewe ni wa thamani sana mbele za Mungu.

leo hii Mungu Katika makanisa amewawekwa viongozi wake ili waweze kukufanya uwe wa thamani sawa na vile ambavyo YEYE amekukusudia.

Kama mtu amepewa Neema na Mungu ya kuongoza, hatuhitaji kuangalia ukabila wake bali tunatakiwa kuangalia kile ambacho amepewa na Bwana. Kila mtu ana Neema na kipawa chake kutoka kwa Mungu.

Siku moja Bwana Yesu alikuwa akitoa mfano na akasema “Kulikuwa na mfarisayo mmoja na mtoza ushuru, wote walikwenda kanisani, yule mfarisayo alikwenda madhabahuni na kuomba, akasema “Ee Mungu mimi sikama yule mtoza ushuru aliyeko kule mlangoni mimi ninakutolea Zaka kila siku” yule mtoza ushuru aliposikia hayo akapiga magoti na kumwambia Mungu “Ee Mungu mimi ni mwenyedhambi ninaomba unisamehe”. Bwana Yesu akasema kuwa yupi aliye sikiwa na Mungu? ni yule mtoza ushuru aliye jinyenyekesha mbele zake. Mungu anapenda sana wale watu ambao ni wanyenyekevu ambao wanajishusha mbele zake, ukiwa ni mmoja wao Mungu anaweza kukuinua na kukufikisha kiwango cha juu zaidi.

Jishushe na unyenyekee mbele za Mungu ili kwamba yeye aweze kukuinua.

MAMA ELIAKUNDA MWINGIRA – IBADA DEC 3 -2017

Zaburi 34:1-10 “Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi. Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja. Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya. Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote. Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu. Wana-simba hutindikiwa, huona njaa; Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema. ”
Inapendeza kumshukuru Mungu kuliko hata kuomba, unapo onyesha moyo wa shukrani kwa Mungu ni sawa na unaruhusu Mungu afanye jambo jipya kwako, unapo onyesha moyo wa Shukrani kwa Mungu, unamfanya Mungu afanye mambo makubwa zaidi kwako.

Daudi alijifunza kuimba na kumtukuza Bwana na hiyo ikamfanya Mungu amfurahie, unapokuwa na moyo wa shukrani unamfurahisha Mungu.

Unapo msifu na kumtegemea, unamfanya kushawishika kufanya kitu kwako, unaruhusu Mbingu isilale kwa ajili yako. Daudi akasema “Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.” Usiangalie yanayo kuzunguka muinue Bwana nawe utamuona katika maisha yako.

Zaburi 34:3 “Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja.” Furahi na hao walio tendewa miujiza kwa sababu muujiza wako unakuja. Upendo unaleta uponyaji.

Usiangalie mazingira bali muangalie Mungu alivyo mkuu, Yeye ni wa UPENDO na wa REHEMA anaweza kukurehemu. 
Mungu wetu ni Mungu aliye hai anatenda maajabu kila iitwapo leo, inua sifa kwa Bwana usiangalie mazingira yanayo kuzunguka kuwa ni magumu kiasi gani, Mungu anajua shida yako na anaweza kukuponya. Daudi akasema “Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.” Je! Wewe unamtafuta Bwana? Kama unamtafuta Bwana atakuponya.

Wewe unaye Mtumaini na kumngoja Bwana hakuna siku atakuacha uaibike, kaza macho yako kwa Bwana ipo siku ataiviringisha aibu yako nawe utashuhudia matendo makuu aliyo kutendea.

“Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.” Bwana amesikia mateso yako, na sasa zamu yako imefika atakutoa katika taabu zako, unatakiwa kumtumaini Yeye tu, hajawahi kushindwa na chochote, anaweza yote.

Zaburi 34:7 “Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.” Malaika wa Bwana wako kazini wako mahali ulipo ili kukuokoa, hutakufa bali utaishi, hautaaibika bali utaheshimika.
“Onjeni muone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.” Katika kumtegemea Bwana hatakuacha kamwe. Kila inapoitwa leo utakuwa na wimbo mpya kinywani mwako, na utakuwa na ujasiri wa kusema Bwana ni mwema maana atakuwa mwema kwako. Ibilisi analijua hilo na ndio maana anakujaza uchungu ili usiweze kupokea Baraka zako. Nilipolitambua hilo niliamua kutoa machungu yote moyoni mwangu na kuamua kumuweka Yesu tu.
Toa machungu moyoni mwako, usimuweke mume, biashara au watoto katika moyo wako, ukifanya hivyo ni sawa na umeweka misumari katika moyo wako. Moyoni mwako muweke Yesu maana yeye hatakuumiza, na ndio maana akasema “mwanangu nipe moyo wako”, mpe moyo wako Bwana Yesu, maana yeye hataweza kukuumiza bali utakuwa salama.

Ukimuweka Yesu moyoni mwako utaweza kuwaza au kuona sawa sawa na vile ambavyo Mungu alikukusudia na ndipo utasababisha USTAWI katika maisha yako. Siku hizi kuna magonjwa mengi sana, kwa sababu ya msongo wa mawazo, ukiamua kumuweka Yesu moyoni mwako badala ya machungu na magonjwa kukaa ndani yako unakuwa na furaha na amani tele na unakuwa salama.
Mimi nilikuwa ni mtu anayejua kuweka vitu moyoni ila baada ya kuamua kumuweka Yesu moyoni mwangu sasa nina Amani na furaha tele, jaribu na wewe uone ya kuwa Bwana yu mwema.

MCHUNGAJI AIMANA DOMINICK – IBADA DEC 3 – 2017

Usipotangaza kuwa Yesu anaponya inamaana unausukumia mbali ule uponyaji wake, lakini unapotangaza kuwa Yesu anaponya unaruhusu ile nguvu ya uponyaji kukujia.
Kutoka 15:26 “ Akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa MIMI NDIMI BWANA NIKUPONYAYE”.

Mungu ametuhakikishia kwenye ahadi zake kuwa Yeye yupo ili kutuponya. Mungu hayupo ili kukuangamiza au ili kuharibu ndoa yako, bali yupo ili KUKUPONYA, kuponya ndoa yako, biashara yako, kazi zako na akili yako. Kama huyu MPONYAJI yuko kwa ajili yako basi wewe leo anza kutangaza UPONYAJI wako hata kabla haujatokea maana kadri unavyotangaza ndivyo unavyo harakisha kutokea kwake.

UPONYAJI sio kwa ajili ya jirani yako bali ni kwa ajili yako. Uponyaji wa Mungu kwako uko karibu sana zaidi ya unavyo fikiria, wewe unaona kama kuponya uko mbali kwa sababu umekuwa mwepesi kutangaza tatizo lako zaidi ya kutangaza UWEZA wa Mungu katika KUPONYA.
Kuanzia leo anza kutangaza kuwa Yesu ANAPONYA na utaona UPONYAJI ukitokea katika maisha yako.

Amri kutoka kwa Bwana Yesu ni sisi TUPONYEKE na si tuumwe, unatakiwa utangaze kuwa Yesu anaponya, kwa sababu kwa kadri unavyo endelea kutangaza ndivyo lile tangazo linavyo endelea kutimia kwako.

” KWA KUWA MIMI NDIMI BWANA NIKUPONYAYE.”  Hii ni AHADI ya Mungu kwetu sisi, mpango wake ni KUTUPONYA, unapaswa kuelewa hili katika akili yako; katika mazingira yeyote unayo pitia YEYE anasema kuwa anaponya, hata kama shida yako unaiona kuwa ni kubwa sana lakini bado unapaswa kujua kuwa YEYE ANAPONYA.

Uponyaji uko hapo hapo ulipo, lakini tatizo ni kuwa haupokei kwa sababu haujui ni jinsi gani unaweza kuutumia. Mfano:- Unaweza ukawa na simu ya mtu na hauwezi kuitumia, unaweza kushinda nayo tangu asubuhi hata jioni, hata kama inapesa lakini kama huwezi kuitumia hutaweza kufanya chochote hata kama unashida. Hivyo ndivyo ilivyo kwetu, kila mmoja wetu ana Roho Mtakatifu ndani yake, na anauwezo wa kuwasiliana naye, lakini wakati mwingine kwa sababu ya maneno ya wanadamu ya kushindwa waliyokwambia unaona kuwa haiwezekani, unapaswa kujua kuwa inawezekana; imba kuwa Yesu anaponya.

Kile unacho kitamani ni cha kwako ni wewe tu kujua kuwa hiki ni changu, YEYE anasema kuwa “NI MUNGU AKUPONYAYE” anatamani kukuponya, kwa nini hauponyeki? Tatizo ni mashaka uliyo nayo. Unapaswa kujua kuwa Mungu ANAWEZA yote.

SEMINA YA MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU, EFATHA MINISTRY MWENGE DAR ES SALAAM,

 

MCHUNGAJI: ANGELINA MDADILA

Mungu alipomtuma Musa ili kuwatoa wana wa Israel Misri, Mungu huyo huyo  alikuwa anaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Kwa nini alisema hivyo? Kwa sababu alikuwa anataka kujitwalia Utukufu.

Kutoka 14:5 “Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena?

Unapo pokea uponyaji unapaswa kuwa makini kuulinda uponyaji wako kwa sababu shetani anapotoka kwa mtu huwa anarudi kuangalia kama pale ambapo ametoka umepajaza!. Lakini kama akirudi kwako na kukuta dhambi ndani yako anafurahi maana anarudi tena kwa nguvu kuliko hata mwanzo. Unapaswa kuwa makini kwa sababu ibilisi si mjomba wala shangazi yako.

Usijisahau unapopokea kitu kutoka kwa MUNGU, unapaswa kuwa na Adabu.

Kutoka 16:3 “Wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.

Baada ya kuvuka usianze kuwaza ulikotoka, maana hata hapo ambapo unaona kuwa hakuna chakula, nguo wala chochote pana njia maana ni kwa kusudi la Mungu uko hapo.

Ukiwa na Ushirika na Roho atakuelekeza hatua kwa hatua.

Usije ukamchanganya Mungu, usiombe pesa kwa ajili ya kitu kingine na ukafanyia kitu kingine itakuwa ni sawa na umefanya kosa la jinahi kwa Mungu.

Mungu ANAWEZA, kama UMEMUOMBA jambo lolote lile USIWE na MASHAKA, unachotakiwa ni wewe KUAMINI tu  kuwa YEYE ANAWEZA, naye ATAKUTENDEA.

Unatakiwa kutii maagizo, kuwa na ushirika na Roho Mtakatifu na kuishi maisha Matakatifu, hayo yatakusaidia kushinda dhambi katika maisha yako.

Wana wa Israel walipokuwa wanashushiwa mana na Mungu walikuwa wameambiwa kuwa kwa siku tano wachukue chakula cha siku moja moja na siku ya sita  wachukue cha siku mbili, lakini wao walikuwa wanachukua hata cha siku mbili siku zile walizoambiwa wachukue siku moja.

Kutoka 16:25-27 “Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya Bwana; leo hamtakiona nje barani. Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana.  Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione.

Wana wa Israel walikosa utii, kwa sababu hiyo ikawafanya wakazunguke jangwani kwa miaka yote hiyo 40, waliteseka kwa sababu ya kuto kutii. Hivi  ndivyo ilivyo kwetu sisi leo tumepokea kutoka kwa Mungu tangu tulipo anza kuomba lakini yanashindwa kudhihirika kwa sababu ya kuto kutii kwetu

Kutoka 15:26 “Akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye. Ukitii sheria za Bwana hataweka tena magonjwa kwako.

Warumi 2:22-29 “Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu? Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati? Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa. Kwa maana kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa? Na yeye asiyetahiriwa kwa asili, aishikaye torati, je! Hatakuhukumu wewe, uliye na kutahiriwa, ukaihalifu torati? Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili;  bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu. ” 

 

 

MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA – NOV 26 – 2017

Leo ni siku yako ya kubadilishwa;

Siku zote Mungu anaiangalia siku, kwa sababu yeye hayuko katika wakati wala majira, Mungu ni Mungu na matendo yake yanaelekezwa kwa siku, wewe ndio unaye tazamia wakati na majira lakini ndani yake hakuna majira, Yeye ni yule yule jana leo na hata milele.
Hii inamaana gani? Inamaana jinsi alivyokuwa jana ndivyo hivyo hivyo alivyo leo, na kama alivyo leo ndivyo atakavyokuwa kesho, Mungu wetu habadiliki, wewe unaweza kubadilika lakini Yeye kamwe hata badilika. Wewe unaweza kubadilika na unatakiwa kubadilishwa ili kwamba uweze kutembea pamoja naye na ili uwe tayari kwa ajili yake.
Yeye yupo tayari kwa ajili yako, Je! Wewe uko tayari kwa ajili yake?

Mathayo 14:22-27 “Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. ….. ”
Yesu akawaambi wanafunzi wake nendeni mbele kule ambako aliwaagiza waende, lakini katikati ya safari YESU akatokea kutoka kule mlimani alikokuwa akiomba peke yake. Siku unapotaka kuomba mbele za Mungu haijalishi ni watu wangapi wamekaa kando yako unapaswa kuwa peke yako, Mungu anapenda watu ambao wako peke yao. Wasahau wale walio kando yako na ujitazame wewe mwenyewe. Usimwangalie mume/mke wako, au ndugu yako aliye kaa jirani yako bali jiangalie mwenyewe na utamwona Mungu leo.

Yesu alitoka kule Mlimani akiwa tayari KUDHIHIRISHA NGUVU za MUNGU, huwezi kupata NGUVU za MUNGU mpaka uwe Mlimani na ukiwa peke yako. Tamani uwe peke yako ukiwa mbele za Mungu.
Baada ya maombi yale Yesu akatoka akiwa na UDHIHIRISHO wa NGUVU za MUNGU, unapotoka Mlimani unakuwa na uhakika wa NGUVU za MUNGU. Baada ya Yesu kufika kwa wanafunzi wake “akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Siku ya leo ninakwambia kuwa USIOGOPE maana kuna kitu kitakutokea katika maisha yako, jiandae kupokea muujiza wako.

2Wafalme 4:18-37 “Hata yule mtoto alipokua, ikawa siku moja alitoka kwenda kwa baba yake kwenye wavunao. Akamwambia baba yake, Kichwa changu! Kichwa changu! Naye akamwambia mtumishi wake, Mchukue kwa mama yake. Akamchukua, akampeleka kwa mama yake, naye akakaa magotini mwake hata adhuhuri, kisha akafa………..”

Watu wengi hapa Duniani wako katika mazingira haya inawezekena ukawa ni wewe, huyu mwanamke mshunami ambaye mtoto wake alikufa, alijitambu hivyo akasema kuwa hahitaji kulia. Alijua kuwa mtoto alitoka kwa Mungu hivyo akajua kuwa Mungu anaweza kufanya jambo kwa ajili ya mtoto wake.
Yule mtoto alikuwa amekufa lakini yule mwanamke alikataa kulia na kukubaliana na ile hali ya kifo cha mtoto wake, alijua wapi pa kwenda maana alijua kuwa mtoto alitoka kwa Mungu. Ndipo alipochukua punda na mjakazi na kumwambia kuwa afanye haraka ili kuwahi kwa Mtumishi wa Mungu. Unapotaka kitu kitokee kwako fanya haraka kuwahi kwenye uwepo wa Mungu, maana Mungu wetu si mvivu hivyo unapaswa kufanya haraka ukitaka kitu kutoka kwake.

 

MCH. COSTANTINE MASSAWE – IBADA NOV 27 – 2017

Yeremia 32:27 “Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza? ”. Je wewe unashida ambayo Mungu hawezi kuitatua?
Sahau shida, ugumu na mambo yanayo kutesa kwa sababu Mungu anauwezo wa kulikabili tatizo lako, unachopaswa kutambua ni kumkumbatia MUNGU maana yeye anajua haja ya moyo wako, fungua moyo wako kwake na utamuona akikutetea. ungu wetu anauweza mkuu juu ya ugumu wa maisha yako na juu ya matatizo uliyonayo maadamu tu wewe unamwili. Unapaswa kutambua kuwa sasa ni wakati wako wa kutolewa kwenye magumu, wakati unaona kuwa mambo ni magumu kwako ndipo Mungu anakwenda kutumia huo ugumu kwa ajili ya utukufu wake.

Sahau shida, ugumu na mambo yanayo kutesa kwa sababu Mungu anauwezo wa kulikabili tatizo lako, unachopaswa kufanya ni kumkumbatia MUNGU maana yeye anajua haja ya moyo wako, fungua moyo wako kwake na utamuona akikutetea.