MAMA ELIAKUNDA MWINGIRA – IBADA DEC 3 -2017

Zaburi 34:1-10 “Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi. Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja. Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya. Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote. Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu. Wana-simba hutindikiwa, huona njaa; Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema. ”
Inapendeza kumshukuru Mungu kuliko hata kuomba, unapo onyesha moyo wa shukrani kwa Mungu ni sawa na unaruhusu Mungu afanye jambo jipya kwako, unapo onyesha moyo wa Shukrani kwa Mungu, unamfanya Mungu afanye mambo makubwa zaidi kwako.

Daudi alijifunza kuimba na kumtukuza Bwana na hiyo ikamfanya Mungu amfurahie, unapokuwa na moyo wa shukrani unamfurahisha Mungu.

Unapo msifu na kumtegemea, unamfanya kushawishika kufanya kitu kwako, unaruhusu Mbingu isilale kwa ajili yako. Daudi akasema “Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.” Usiangalie yanayo kuzunguka muinue Bwana nawe utamuona katika maisha yako.

Zaburi 34:3 “Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja.” Furahi na hao walio tendewa miujiza kwa sababu muujiza wako unakuja. Upendo unaleta uponyaji.

Usiangalie mazingira bali muangalie Mungu alivyo mkuu, Yeye ni wa UPENDO na wa REHEMA anaweza kukurehemu. 
Mungu wetu ni Mungu aliye hai anatenda maajabu kila iitwapo leo, inua sifa kwa Bwana usiangalie mazingira yanayo kuzunguka kuwa ni magumu kiasi gani, Mungu anajua shida yako na anaweza kukuponya. Daudi akasema “Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.” Je! Wewe unamtafuta Bwana? Kama unamtafuta Bwana atakuponya.

Wewe unaye Mtumaini na kumngoja Bwana hakuna siku atakuacha uaibike, kaza macho yako kwa Bwana ipo siku ataiviringisha aibu yako nawe utashuhudia matendo makuu aliyo kutendea.

“Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.” Bwana amesikia mateso yako, na sasa zamu yako imefika atakutoa katika taabu zako, unatakiwa kumtumaini Yeye tu, hajawahi kushindwa na chochote, anaweza yote.

Zaburi 34:7 “Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.” Malaika wa Bwana wako kazini wako mahali ulipo ili kukuokoa, hutakufa bali utaishi, hautaaibika bali utaheshimika.
“Onjeni muone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.” Katika kumtegemea Bwana hatakuacha kamwe. Kila inapoitwa leo utakuwa na wimbo mpya kinywani mwako, na utakuwa na ujasiri wa kusema Bwana ni mwema maana atakuwa mwema kwako. Ibilisi analijua hilo na ndio maana anakujaza uchungu ili usiweze kupokea Baraka zako. Nilipolitambua hilo niliamua kutoa machungu yote moyoni mwangu na kuamua kumuweka Yesu tu.
Toa machungu moyoni mwako, usimuweke mume, biashara au watoto katika moyo wako, ukifanya hivyo ni sawa na umeweka misumari katika moyo wako. Moyoni mwako muweke Yesu maana yeye hatakuumiza, na ndio maana akasema “mwanangu nipe moyo wako”, mpe moyo wako Bwana Yesu, maana yeye hataweza kukuumiza bali utakuwa salama.

Ukimuweka Yesu moyoni mwako utaweza kuwaza au kuona sawa sawa na vile ambavyo Mungu alikukusudia na ndipo utasababisha USTAWI katika maisha yako. Siku hizi kuna magonjwa mengi sana, kwa sababu ya msongo wa mawazo, ukiamua kumuweka Yesu moyoni mwako badala ya machungu na magonjwa kukaa ndani yako unakuwa na furaha na amani tele na unakuwa salama.
Mimi nilikuwa ni mtu anayejua kuweka vitu moyoni ila baada ya kuamua kumuweka Yesu moyoni mwangu sasa nina Amani na furaha tele, jaribu na wewe uone ya kuwa Bwana yu mwema.

Comments

comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *