SOMO: AHADI ZA MUNGU. (IBADA YA JUMAPILI 28 JANUARI 2018)

Na Mtume na Nabii Josephat Elias. Mwingira.

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea NGUVU, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa MASHAHIDI wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Kwa nini NGUVU? NGUVU itatusaidia sisi kuwa mashahidi wa Kristo huku duniani, hivyo usiitamani hiyo NGUVU ili upate pesa bali itamani ili uweze kuwa shahidi; na pale Mungu anapoona tamanio lako ni hilo, atakupa mahitaji yako yote unayo yahitaji ili uweze kuwa shahidi wake huku duniani.

Kwa nini haupati mali toka kwa Mungu? Kwa sababu katika akili yako na moyo wako ile shauku iliyo ndani yako unaitaka hiyo Nguvu ya Mungu ili upate pesa na si ili uweze kushuhudia. Ili yeye aweze kukubariki hoja yako iwe ni kushuhudia si kupokea mali.
Kama msukumo ulio ndani yako ni kutaka kuwashuhudia watu ili wamjue Mungu hiyo NGUVU itakuja kukusaidia mahali popote pale katika maisha yako, iwe ni kwenye ndoa yako, kazini kwako kwenye afya yako n.k. Jionyeshe kuwa umezaliwa mara ya pili kwa matendo na si kwa maneno tu.

Unapo pokea NGUVU za MUNGU ni uhakikisho ya kwamba umezaliwa mara ya pili, mara zote lazima tujionyeshe ya kwamba tumezaliwa mara ya pili, hivyo tunapo pokea hiyo NGUVU ni uhakikisho ya kwamba sisi ni wa Kristo.
Pasipo Nguvu huwezi kushuhudia wala kuwa shahidi bali utakuwa muathilika kwa ibilisi, kwa maana yeye atakutesa na kukufanya uwe hovyo, lakini kama umezaliwa mara ya pili (yaani umempokea Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako) kamwe wewe si mali tena ya ibilisi .
Yohana 16:8 “Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya DHAMBI, na HAKI, na HUKUMU.”
Anapokuja atauhakikishia ulimwengu kwa mambo matatu:-
1. Kwa habari ya dhambi,
2. Haki na,
3. Hukumu.
Hayo maeneo MATATU ni ya MUHIMU sana katika maisha yako kuyajua na kuwa nayo.
Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa wamezaliwa mara ya pili yaani (wameokoka) lakini ibilisi anapokutazama anaona kuwa unafanya mchezo; sasa atakacho kifanya ni kuwa atakuja kwako kuliko alivyokuwa mwanzo ili kukufanya uwe hovyo huku ukiwa umeshikilia Biblia na unakwenda Kanisani.
Kama umeamua kumpokea Bwana Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako maanisha na usijaribu; kwa sababu kama utajaribu ibilisi atakumaliza, hatumfanyii ibilisi mzaha mzaha atakuangamiza na kukufanya uwe hovyo.

Yohana 16:9 “Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi;” Dhambi ni nini? Ni kuto kumwamini Yesu Kristo, dhambi si uzinzi, kunywa pombe, kuiba, kuongea uongo na yale yanayo fanana na haya; yote haya ni matunda ya dhambi. Unapo muona mtu akifanya hayo mambo haijalishi kuwa anakwenda Kanisani jua kuwa huyo mtu hana Yesu na hajazaliwa mara ya pili, anajaribu kuzaliwa mara ya pili.

1Yohana 3:7-10 “Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi …”
Ni nani mwenye haki? Ni Yesu Kristo na yeyote anayetenda kwa haki jua kuwa huyo ni wa Yesu. Atendaye dhambi ni wa Ibilisi na Yesu atakapokuja mtu huyo hatakwenda Mbinguni, kama wewe ni mmoja wao tubu sasa acha kujifariji kwani usipo tubu utaenda jehanam ukiwa Kanisani.
Yeyote aliyezaliwa mara ya pili yuko nje ya uangamizi wa Ibilisi, na ibilisi hana nguvu juu yake. Kwa nini unapokuwa umezaliwa mara ya pili dhambi haina nguvu juu yako? Kwa sababu Kristo amezaliwa ndani yako na yeye alisha shinda dhambi.

Yohana 16:9-10 “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.”
Hakuna aliye zaliwa mara ya pili na anatenda dhambi, kama unatenda dhambi acha kupoteza muda kwenda Kanisani ili kujificha nenda kule wanako kwenda wale wafanyao dhambi. Kanisani ni mahali pa watakatifu wa Mungu ili waweze kuzidhihirisha NGUVU za Mungu sio kuzionyesha kazi za ibilisi bali kuziharibu kazi za ibilisi.

Maana ya dhambi ni kuto kumjua Yesu, kama unamjua Yesu inamaana kuwa umezaliwa mara ya pili na unatembea katika HAKI ya Mungu. Je unaenenda katika haki ya Mungu? Je unaishi katika UTAKATIFU?.

Comments

comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *