SOMO: KUVUKA NG’AMBO YA PILI

ASKOFU: CHALRES KARIUKI – KENYA

Baada ya Yesu kuhubiri kukawa usiku, akauacha mkutano na kuwaambia wanafunzi wake wavuke ng’ambo. Marko 4:35 “Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo.” Kule ng’ambo kuna vitu vikubwa sana.

Kuna mambo unapaswa kuyafahamu:-
• Maarifa; nini maana ya maarifa? Ni kukusanya taarifa, yaani unakuwa na taarifa. Mtu anapokwenda shuleni kusoma inamaana kuwa anakusanya taarifa, lakini katika ile shule kuna kuhitimu na baada ya kuhitimu yule mwanafunzi anapewa nguvu ya kwenda kufanya yale ambayo amejifunza. Leo ni siku ya kuhitimisha, Mungu aliye Baba yetu atatupa Nguvu ya kwenda kutekeleza yale tulio jifunza.
• Ufahamu; Ufahamu ni ile hali ya uelewa wa taarifa. Watu wengi wanakwenda shule na kupata Maarifa lakini hawapati Ufahamu. Ukapate ufahamu katika Jina la Yesu
• Hekima; Hekima ni nini? Ni ile hali ya kukuwezesha kutenda kazi kwa vitendo, Maarifa na Ufahamu. Unapo anza kutendea kazi kwa Maarifa na Ufahamu ndipo unapokea Hekima. Bwana akakupe uwezo wa kutekeleza Maarifa na Ufahamu ili uweze kupokea Hekima.

Marko 4:35 “Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo.” Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake na tuvuke ng’ambo.
Kule Upande wa pili, Upande wa ng’ambo ni wa Ushindi, hakuna kushindwa bali ni upande wa kushinda.
Mungu akamwambia Musa wewe uko ukingoni mwa Bahari, hawa watu wa Ibrahimu lazima waivuke hiyo Bahari ya Shamu mpaka ng’ambo ili waweze kurithi. Musa aliwaongoza wana wa Israel kuelekea nchi ya Ahadi. Wale ambao ulikuwa ni uzao mchanga walikuwa ni uzao wa Yoshua na Kalebu, lakini uzao uliotoka Misri ulikufa jangwani. Hivyo ilimbidi Musa na yeye afe ili ule uzao mchanga uweze kufika katika nchi ya Ahadi.

Yoshua 12:7 “Hawa ni wafalme wa hiyo nchi ambao Yoshua na wana wa Israeli waliwapiga ng’ambo ya pili ya Yordani upande wa magharibi, …. ”
Walipokuwa ng’ambo ya Yordani Musa aliwapiga wafalme wawili, Sihoni mfalme wa Waamori na Ogu Mfalme wa Bashani ili kumuonyesha Yoshua njia na ili kumfundisha Yoshua kuwa si yeye atakaye wapigania Israel watakapo vuka Yordani bali ni Mungu. Upande wapili wa mto Yordani kulikuwa kuna vitu vingi vya kumiliki.

Baada ya kuvuka Yordan nchi ya kwanza kuweza kuimiliki ni Yeriko maana ilikuwa imefungwa, lakini Mungu aliwapa kuimiliki kwani aliwawezesha wao kuingia ndani. Upande wa ng’ambo kuna adui wamekalia Mbaraka wako lakini utakapovuka usihofu kwa sababu upande wa ng’ambo Mungu atakufanya Ustawi, kwa sababu chochote kile ambacho adui yako amekalia ni cha kwako.

Kuna vitu ambacho walipaswa kumiliki Babu zako au wazazi wako lakini hawakumiliki kwa sababu walikuwa ng’ambo ya Yordani hivyo kwa kuwa wewe Mungu amekuvusha kila ambacho Mungu aliwapa babu zako au Baba yako na hawakumiliki ni cha kwako, wao hawakumiliki kwa sababu walikufa wakiwa upande wa pili wa Yordani. Mimi na wewe tunavuka ili kumiliki nchi yetu ya Ahadi. Baba zetu walifia jangwani ili sisi tuweze kumiliki nchi ya Ahadi.

Bwana Yesu aliuchukua umaskini wetu na kuupeleka msalabani na alipokuwa anasurubiwa alisema imekwisha. Pale msalabani umaskini wako ulishindwa, pale msalabani ulipata haki yako ya kumiliki , pale msalabani ulipokea afya njema na kila kitu unacho kihitaji katika maisha yako. Ibilisi ni muongo na hauelewi msalaba kwa sababu msalaba ni kwa ajili ya kuvuka, kuacha kila shida au matatizo na kuwa mzima na kumiliki.

Biblia inasema alichukua udhaifu wetu ili mimi na wewe tusishindwe, Yesu Kristo alisulubiwa kwa sababu msalabani alifuta hatia zetu, laana, alifuta kushindwa kwetu na akatupa kushinda.

Ng’ambo utakuwa mmiliki, kwa sababu kule ng’ambo si upande wa Baba yako bali ni upande wa Baba yetu wa Mbinguni ambaye Mbingu na nchi ni mali yake hivyo atakupa kumiliki.

 

Comments

comments

Comments are closed.