SOMO: NGUVU YA MUNGU, (IBADA YA JUMAPILI FEB 11- 2018)

MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA;

1Yohana 5:4-6 “Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu. Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu. Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli. Kwa maana wako watatu washuhudiao mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja. Kisha wako watatu washuhudiao duniani, Roho, na maji, na damu; na watatu hawa hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe.”

Neno lolote niwafundishalo siyo mapenzi yangu bali ni mapenzi yake BABA wa Mbinguni.

Mwaka huu ni mwaka wa NGUVU, mtu akiwa na NGUVU USHINDI ni wa kwake, mfano; kwenye eneo la mapambano yeyote mwenye NGUVU kuliko mwingine ndiye atakaye kuwa mshindi; au kwa wanariadha yeye mwenye nguvu kuliko wengine ndiye atapata medali ya dhahabu, USHINDI unatokana na NGUVU, mnyonge kamwe hatawahi kuwa MSHINDI; NGUVU ndiyo msingi wa USHINDI wetu.
Mara zote walio wanyonge wanashindwa kwa sababu ya unyonge wao, mwaka huu Mungu ameridhia tupate NGUVU zake ili tupate KUSHINDA.

Nguvu ndiyo msingi wa USHINDI, hivyo unahitaji nguvu katika akili zako, mawazo yako, maamuzi yako, kwenye biashara zako ili uweze kushinda, mara nyingi unapata hasara kwa sababu wewe ni dhaifu katika biashara yako, au umepewa talaka kwa sababu ni dhaifu katika ndoa yako. Hujaoa kwa sababu huna nguvu ya kusababisha wadada wakupende au hujaolewa kwa sababu huna nguvu ya kuwavuta wakaka wakuoe, huwezi kupata mtoto kwa sababu huna nguvu ya kutengeneza mtoto.
Nguvu ni nini basi? Ni kile unacho kihitaji, yaani ni kiwezesho cha kupata kile unacho kihitaji. Nguvu ni ya muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku.

Nguvu ni nini? Zaburi 62: 11 “Mara moja amenena Mungu; Mara mbili nimeyasikia haya, Ya kuwa nguvu zina Mungu,”  Nguvu ni ya MUNGU na inamilikiwa na YEYE tu, nani anaibeba hiyo nguvu?  Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” inamaana kuwa huwezi kupata Nguvu kama Roho Mtakatifu hayupo pamoja nawe maana yeye ndiye anaye beba hiyo NGUVU, pasipo Nguvu huwezi kushinda chochote.

Nguvu ya uovu itakupeleka kuzimu, unaweza kuifurahia hapa kwa kitambo tu lakini utaishia kuzimu kwa sababu waovu mwisho wao ni shimoni.

1Yohana 5:4 ‘Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.’ NGUVU ya MUNGU ni kwa ajili ya kukusaidia wewe kupata USHINDI, ushindi ambao tunauhitaji ni wa kushinda ulimwengu si kushinda mbingu.

Kwa nini tuushinde ulimwengu? 1Wakorintho 2:1-5 “Basi, ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima. Maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa.Nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi. Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.” Inamaana kuwa nguvu hii imetujia kupitia Roho Mtakatifu, je! tunampataje huyo Roho? Kwa kupitia imani; tukiwa na Imani tunaweza kumpokea Roho Mtakatifu, lakini bila imani hatuwezi kumpokea Roho Mtakatifu ambaye ndiye mbeba nguvu za Mungu. Tukimpokea Roho Mtakatifu inamaana kuwa tunayo NGUVU na tunaweza kuidhihirisha NGUVU ya Mungu huku duniani.

Kwa nini tuushinde ulimwengu? Kwa sababu huku duniani kuna mkuu wa anga anaye miliki Dunia, hivyo ili tuweze kushinda tunahitaji NGUVU ya Mungu.  Waefeso 2:1 “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;”
Inamaana kuwa ulimwengu huu una namna ya maisha na kuna mkuu wa anga akiitawala dunia akiwamiliki watu na akiwatumia hao watu kwa ajili ya mapenzi yake mwenyewe. Yeye anawatumia huku akiwatesa, akiwatishia, akiwafanya wawe na maradhi, washindwe, wasiwe na thamani, wawe hovyo na wasio na muelekeo.

Mkuu wa anga anamiliki dunia na anafanya kile ambacho anakitaka huku duniani, bila NGUVU ya MUNGU huwezi kumshinda. Wakati mwingine unakuta mtu anatamani kufanya jambo lakini hawezi; kwa nini? Kwa sababu Yule mkuu wa anga hajamruhusu, mpaka ujitoe au kujisalimishe kwake. Sasa sisi tulio wana wa MUNGU ili tuweze kushinda ulimwengu na tuweze kumiliki tunahitaji NGUVU ya MUNGU ili tuweze kuushinda ulimwengu huu na kutuwezesha kumiliki hapa Duniani. NGUVU YA MUNGU NI YA MUHIMU SANA KATIKA MAISHA YAKO.

Zaburi 106:37 “Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani.” Huyu mkuu wa anga anakufanya wewe kupata njia ambayo utafurahia ya dunia, atakwambia uwatoe watoto wako, wazazi wako na hata ndugu zako ili kwamba upate mali, ndiyo unaweza ukafanya hivyo na ukafanikiwa lakini unapaswa kujua kuwa ni kwa kitambo kidogo tu na mwisho wako ni Jehanam ya moto wa milele.
Unakuta watu wana mali nyingi sana lakini hawataki kumwabudu Mungu na ukiwaambia waokoke hawataki hata kusikia habari ya wokovu, kwa nini? Kwa sababu wao ni watumishi wa mkuu wa anga na kuzimu ndipo mahali pao pa milele. Unaweza kuwaona wanamafanikio na vyote wanavyo vihitaji, ndio wamefanikiwa lakini katika mafanikio mabaya. Uliye mwana wa MUNGU hayo mafanikio siyo kwa ajili yako kwa sbabau wewe ni wa Mbinguni, hivyo ili ufanikiwe unahitaji NGUVU ya MUNGU.
Waamini wengi wasio jua hayo wanabaki kwenye umaskini, siyo kwa sababu hakuna fedha, la! Bali wanakosa nguvu ya kuwawezesha kupata mali.
Unapoanza kupokea kitu kutoka kwa Mungu, unapaswa kuongeza muda zaidi wa kuomba na kukaa na Roho Mtakatifu, unakuta watu wengi wakisha pata mali wanapunguza kumwabudu Mungu matokeo yake wanaishia katika umaskini. Usichoke kuwa na Roho Mtakatifu bali furahia kuwa naye, maana ni yeye tu atakaye kupa njia ya kufikia mafanikio yako, pasipo yeye huwezi kupata chochote.

1Yohana 5:4 “Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.” Je! Wewe unaimani gani? Imani ya Mungu ina njia ya kuipata nguvu; tutajuaje kuwa una imani ya Kristo Yesu? Utaushinda ulimwengu.

Tatizo lililo kubwa kwa watakatifu wanapokwenda mbele za Mungu wanaongea kuhusu matatizo yao wenyewe hawaongelei Upendo, uzuri, msamaha, rehema, fadhili za MUNGU, haki ya Mungu, hawaongelei kuhusu utakatifu wa Mungu na Neno la Mungu, wokovu, ukombozi wa Mungu; bali mara zote wanaongelea kuhusu ndoa zao, watoto wao, na matatizo yao na mara nyingi wamekuwa wakiongelea kuhusu utendaji wa ibilisi, wachawi, wanaongelea kuhusu familya zao. Hawaongelei kuhusu Mungu.

Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake na kuwaambia kuwa waombe kwa Baba yao wa Mbinguni, Kama unataka kumuona Mungu katika maisha yako, Mara zote ongelea kuhusu Ukuu wake, Upendo wake, unapo yaongelea hayo mbingu itakuwa na wewe na itasababisha kukuletea vitu kutoka Mbinguni.

  • Tunapo ongelea kuhusu BABA wa Mbinguni, inamaana kuwa BABA huyu ni Yule anayejua namna ya kuwalea na kuwatunza watoto wake, anajua kuwatangulia watoto wake, ni BABA anayejua kuwaandalia vitu vizuri watoto wake.
  • Baba huyo ni mume wa wajane, anawapigania anawalisha na kuwaponya.
  • Yeye ni BABA wa yatima, anawajali, anawasomesha, anawalisha, anawapa mahitaji yao yote.
  • Baba ninaye muongelea ni mponyaji, ndiyo BABA huyo aliye Mbinguni anawaponya na maradhi mbali mbali.
  • Baba ninaye muongelea ni BABA mwenye msamaha, wenye dhambi wanajua, walikuwa wanateseka na dhambi lakini YEYE aliwasamehe, laana ilikuwa juu yao lakini walipomkimbilia YEYE aliwasamehe na wamejazwa na Roho Mtakatifu.

Ibilisi hana kitu chochote hapa duniani ila anacho kitumia ni ujinga wako wa kutokujua nini cha kufanya ili yeye akae mbali na wewe.

Nini ufanye ili yeye akae mbali na wewe?

  • Hakikisha unaishi maisha ya Utakatifu, kwa sababu Utakatifu ni tabia ya Mungu, ukiishi maisha hayo itasababisha Roho Mtakatifu atakaa ndani yako; na yeye akiwa ndani yako USHINDI kwako umehakikishiwa. Hakuna kitakacho sababisha uharibifu kwenye maisha yako tena. Bwana Yesu akasema kwa wewe kulinda utakatifu wako, kama mkono wako unakufanya utende dhambi kata, kama ni jicho lako ling’oe, hii inamaana kuwa utakatifu ndiyo msingi na ndiyo maana Yesu alikufa msalabali ili sisi tupate Utakatifu. Ni Utakatifu peke yake ndiyo unafukuza dhambi ikae mbali na wewe,

Mungu amekupa wewe kuchagua kati ya Utakatifu au uovu, sasa ni kazi yako wewe kuchagua, kama unataka nguvu ya uovu itafute utaipata ila jua kuwa kuzimu kunakusubiria. Lakini kama unataka kwenda Mbinguni hakikisha unafanya chochote kile ili uupate Utakatifu, kaa mbali na dhambi, acha kusema uongo, acha wizi, uwe Mtakatifu, chochote ukipatacho hakikisha unatoa fungu la kumi. Ukawe mwenye haki wa Mungu, kama una watoto wawili au watatu hakikisha mmoja unamtoa kwa Mungu ili amtumikie.

Huwezi kupata nguvu kama haushiki utakatifu na haki ya Mungu.

Je! Unataka ibilisi akae mbali na wewe? Hakikisha unapo amka asubuhi fikiri ni jinsi gani utakwenda kuutunza utakatifu wako, hakikisha unapotoka nyumbani kwako tunza kinywa chako kisinene uongo, iambie miguu yako isiende mahali popote pale ambapo Mungu hajakuruhusu, yaambie macho yako yasiangalie uovu, yaambie masikio yako yasisikilize uovu, kisha sema na nafsi yako iwajibike kwa Mungu.  Kwa kufanya hivyo inakusaidia wewe kupata NGUVU na chochote utakacho kifanya kitastawi na kufanikiwa.

Anza leo kuishi maisha MATAKATIFU na kutunza UTAKATIFU wako.

Comments

comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *