Posts

Mahubiri ya Jumapili Agosti 6. 2017

SOMO : SALA YA BWANA (Muendelezo)

Katika Dunia hii kama HUJITAMBUI wewe ni nani hutakaa utende kama unavyotakiwa kutenda bali utatenda kama mtumwa, na Utatembea hapa duniani kama Mgeni, lakini ukijua wewe ni nani utatembea hapa duniani sawasawa na KUSUDI LA MUNGU katika Maisha yako. Shetani ni muongo atatumia KUTOKUJITAMBUA kwako ili kukutesa na kukufanya wakati wote utembee kama mtumwa na kuishi kama Mgeni katika Dunia hii.

Unapaswa kujua kuwa wewe sio mtumwa au mgeni kwa sababu Mungu alikuumba kwa SURA na MFANO na wake na kukuweka huku duniani uwe Balozi wake akijua utamwakilisha YEYE hapa Duniani, hivyo acha kutembea kama mgeni hapa Duniani. Haijalishi ELIMU, UMRI au JINSIA uliyonayo, unachotakiwa kujua wewe ni MWAKILISHI wa Mungu hivyo Unapotembea na Unapoongea, ongea mambo ya Msingi ukijua UNAMWAKILISHA Mungu. Unapotembea usitembee kama mtumwa, usiongee kama MPUMBAVU bali ongea kama Mtu mwenye HEKIMA ya MUNGU.

Ishi kama MTAKATIFU na Mwakilishi wa MUNGU, badilisha TABIA yako na namna Unavyowaza, maana Mungu hatakaa ajidhihilishe kwako mpaka Utakapobadilisha namna ya Kuongea kwako. Mungu ana Lugha yake, na hiyo Lugha ipo katika Biblia; jifunze KUTENDA au KUONGEA sawa sawa na Biblia inavyosema.

Musa alipokufa Mungu hakumpa Yoshua njia mpya za kutembea na YEYE bali Mungu alimwambia Yoshua aende sawasawa na MAAGIZO ya Musa Mtumishi wake.

Leo Mungu ana Watumishi wake ambao Amewaweka ili KUKUELEKEZA kuhusu HABARI ZAKE ili Wakusaidie kufanya SAWASAWA na Neno linavyosema, unapaswa KUWASIKILIZA Wanachokuelekeza. Kwa sababu kwa kufanya hivyo unasababisha Mbingu kukusaidia katika kila kitu huku Duniani, lakini Usipowasikiliza DUNIA ITAKUFUNDISHA jinsi ya Kutembea na mkuu wa dunia hii.

Mathayo 6:9 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,”

KUNA MUHIMU GANI WA SISI KULIELEWA JINA LAKE?
Ni kwa sababu ndani ya hilo JINA LAKE kuna Mambo ya Msingi katika MAISHA yetu.

Ndani ya JINA LAKE kuna UPENDO; MUNGU ni PENDO na Aliumba kila kitu katika UPENDO wake. Mwanzo 1:31 “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni Chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.”

Mungu ANATUPENDA na ndiyo maana ALITUUMBA. Huwezi Kugundua au Kuumba kitu chochote kile kama huna UPENDO ndani yako. Watu ambao Biashara zao Zinakuwa (zinaongezeka) jua kuwa wana UPENDO ndani yao juu ya hiyo Biashara, kama una biashara yeyote ile na Haikui au ikafa jua kuwa Huna UPENDO ndani yako.

UPENDO ni Muendelezo hivyo usipokuwa na UPENDO Hutakaa uanze kitu chochote kile na Kikakua, lazima Kitakufa tu hata kama ni NDOA, maana kinakuwa hakina Muendelezo.

Huwezi Kufanya Biashara au Kuanzisha Kampuni na IKASTAWI kama huna UPENDO, maana kunakuwa hakuna MUENDELEZO ndani yako wa kufanya hicho Ulichokianzisha Kukua.

Kama hamna PENDO ndani yako basi hamna UTHAMANI au ile Hali ya kufanya jambo kwa UBORA na UTIMILIFU kwa sababu ndani ya PENDO ndiko kuna UKAMILIFU.

Watu wote wanaojua Kupika vizuri wana UPENDO ndani yao, kama HUJUI Kupika vizuri ujue Huna UPENDO. Kama Mpishi ana PENDO ndani yake, akipika Chakula kinakuwa na ladha Nzuri inayotokana na lile PENDO lililoko ndani yake.

Kama Mke wako HAJUI kupika Tambua kuwa ndani yake hakuna PENDO, kwa sababu inawezekanaje Mke anakwambia ANAKUPENDA na Anakupikia Chakula KIBAYA?

Mke yeyote ANAYEMPENDA Mume wake ATAHAKIKISHA Anampikia Chakula Kizuri Mume wake.

Kama Mume ana PENDO ndani yake ATAHAKIKISHA Anajenga NYUMBA Nzuri ili Mke aweze KUJIVUNIA, ukiona Mwanaume amejenga NYUMBA Nzuri ujue ANAMPENDA Mke wake.

Katika NDOA ndipo Mungu ALIPO na NDIPO Anapoonyesha UUMBAJI wake, hivyo Mume au Mke AKIKAA Vizuri katika NAFASI yake katika hiyo Ndoa kunakuwa na USTAWI maana NGUVU ya Mungu Inakuwepo ndani ya FAMILIA yao.

Kumbukumbu la Torati 28:1-2 “Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako.”

UNAPOSIKIA Maagizo ya Mungu na KUYAFANYA kwa UAMINIFU Mungu aliye BABA yetu atakupa MAHITAJI YAKO yote unayoyahitaji, kamwe huta ya kimbilia ili kuyatafuta bali YATAKUJA, unachotakiwa ni Kumtafuta YEYE.

UTAMTAFUTAJE? Kwa KUTENDA Sawasawa na MAAGIZO Yake kutoka kwa Watumishi wake. Kwa jinsi Utakavyoenda SAWASAWA ndivyo Unavyojiandaa mwenyewe ili Kumpata YEYE.

HUTAWEZA Kumuona Mungu kwa Kufunga usiku na mchana bali UTAMUONA pale Utakapotenda SAWASAWA na Maagizo YAKE, unaweza Ukafunga na Kuomba usiku na mchana atakusikia ndio lakini Usimuone kwa sababu YEYE Anaangalia MATENDO YAKO Kwanza kama ni SAWA na Anavyotaka Wewe UWE au UTENDE, ndipo Atakujibu.

Mungu Anaweza KUKUPA ZAIDI ya Unavyohitaji kama ukitenda sawasawa na MAAGIZO yake, Hatakupa kwa sababu unaomba sana bali kwa KUTENDA SAWASAWA.

Ukifanya mambo ya Mungu SAWASAWA kama Alivyokuagiza OMBA LOLOTE NAYE ATAKUPA.

Mtume na Nabii JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA.

IBADA YA UKOMBOZI NA UPONYAJI KWA DAMU YA YESU, EFATHA MINISTRY MWENGE DAR ES SALAAM.

MASHAKA:
Mashaka yamebeba KUTOKUAMINI, kama unamashaka yeyote moyoni mwako ya kwamba unacho kihitaji kutoka kwa Mungu hutakipata basi ni afadhali usiombe, kwa maana unapokuwa na mashaka hutaweza kupokea.
Endapo utajisemea mwenyewe kuwa haustahili kupokea kitu chochote kutoka kwa Mungu inamaana kuwa hutaweza kupokea, kwa maana umejikataa mwenyewe, lakini ukijikubali utapokea. Mungu anataka watu wanaojitambua kuwa wanastahili, unapokwenda mbele za Mungu unapaswa kuelewa kuwa Mungu anataka uwepo hapo ulipo na yeye anakufurahia, hatakama unadhambi kiasi gani lakini yeye anakufurahia na ndiyo maana akamtoa mwanaye wa pekee Yesu Kristo ili afe kwa ajili yako, inamaana kuwa wewe unastahili machoni pake, yaani wewe ni wathamani sana mbele zake ndiyo maana Mungu hakutaka kukupoteza.
Wewe unathamani sana mbele za Mungu na unastahili kupokea kile unachokiomba kwa Mungu kwa sababu anakupenda.

Ondoa hali ya kutokuamini ndani ya moyo wako ili uweze kupokea kutoka kwa Mungu, Amini kwamba Mungu anaweza kukuponya na kurejesha chochote kilicho haribiwa ndani ya mwili wako, yeye ananguvu za kutenda miujiza kwako, maana yeye ni mtenda miujiza.
Amini ya kwamba Mungu anaweza kurejesha kila kilichoharibiwa ndani ya mwili wako.
Mungu anauwezo wa kukuosha maana yeye ananguvu za kurejesha maisha yako yaliyo haribiwa ili uweze kubeba USHUHUDA kwa ajili ya JINA lake.

Marko 11:19-26 “Na kulipokuwa jioni alitoka mjini. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu….. ”

SALA: Unaposali unapaswa kuamini, nini maana ya kuamini? Kuamini ni kuwa na uhakika wa unacho kiomba, na ni kutambua kuwa kile unacho kiuliza au kukiomba tayari unacho. Unaposali au kuomba Amini kwamba unacho kile ambacho unacho kiomba.
Kuamini kunaanza kabla hujaomba au kuuliza, unapo Amini utapokea kile unachokwenda kukiomba au kuuliza, huwezi kuomba kama huamini. Kabla hujaomba unapaswa kwanza kuamini kuwa Mungu anaweza kukupa kile utakacho kiomba, kama hauamini usiombe maana hutapokea.

MSAMAHA: Kama unataka kupokea kitu kutoka kwa Mungu hakikisha unawasamehe wale waliokukosea, yeyote ambaye unajua mmokosana naye hakikisha unamsamehe kabla hujakwenda mbele Za Mungu ili kuomba.
Msamaha ni kwa faida yako na si kwa yule unaye msamehe, unapo msamehe mtu inamaana kuwa unajisamehe mwenyewe kwa sababu usipo fanya hivyo hutaweza kusamehewa na Mungu, unapomsamehe mtu unakuwa huru. Msamaha ni njia ya kupokea kutoka kwa Mungu, unapojua jinsi ya kusamehe unamruhusu Mungu kukupatia chochote anachotaka kukupa na ibilisi hatakuzuilia kukunyang’anya.

Watu wengi katika dunia hii wanateseka na mambo mengi ikiwemo maumivu na magonjwa, inawezekana umetafuta msaada huku na kule wa kukutoa katika MAUMIVU au MAGONJWA uliyonao lakini haukupata, unapaswa kujua kuwa iko dhambi nyuma yako, yamkini ulifanya wewe au wazazi wako na ndiyo inayokutesa.
Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani. ” Daudi alilitambua hili na ndipo akamsogelea Mungu ili kutaka REHEMA zake, Uko hapo ulipo leo unateseka kwa dhambi ambayo hukuifanya au ulifanya wewe mwenyewe. Unapaswa kujua kuwa dhambi kama dhambi haiondoki wala haifi mpaka imekutana na Damu ya Yesu.

Siyo furaha ya Mungu kwa watu aliowaumba kwa sura na mfano wake wateseke au wahangaike na mateso, FURAHA yake ni kuona WANAFURAHA na SHANGWE katika maisha yao, lakini dhambi ndiyo inayo tesa watu, Mungu hataiondoa mpaka umemsogelea na kutaka REHEMA kwake.

MUNGU HANA UPENDELEO, swali ni Je! unajua kuwa Mungu anaweza kukuponya? Kama unajua kuwa anaweza kukuponya Je! ukotayari? Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” Upo katika UHITAJI lakini NEEMA na REHEMA za Mungu zipo ili kukutoa katika huo uhitaji, unapaswa KUKISOGELEA kiti cha REHEMA kwa UJASIRI ili ukutane na Bwana wa mabwana AKUPONYE na kukutoa katika UHITAJI ulionao.

Mtume na Nabii: Josephat Elias Mwingira.

UJUMBE: JINA

Mtume na Nabii: Josehat Elias Mwingira

Kazi ya Mungu inahitaji UVUMILIVU, KUJITOA, KUWA MAKINI na MOYO WA HURUMA; Kwa sababu pasipo kufanya hayo huwezi kumtumikia Mungu katika ukamilifu.

Mungu ni Roho hivyo huwezi kumuona kwa macho ya DAMU na NYAMA na ni rahisi kumdharau kwa sababu haumuoni.

Usipojua UKUU wa Mungu unaweza ukafanya vitu ambavyo vitamkasirisha na ukasababisha hasira yake ikawa juu yako. Hakikisha kila unachokifanya unaongozwa na Roho Mtakatifu ili hasira ya Mungu isiwe juu yako.

Mathayo 6:9, “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, JINA lako litukuzwe, Ufalme wako uje”.

 1. Kwa nini JINA?

 2. Unaenda kufanya nini na JINA?

 3. Nini kipo katika hilo JINA?

Jina ni la muhimu sana na ndio maana kitu chochote hapa DUNIANI kina jina lake; MITI, MAUA, WANYAMA na vingine vyote vimepewa MAJINA kwa nini? Kwa sababu Jina lolote limebeba uumbaji wa hicho kitu.

Mwanzo 1:26-27, “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. ”

Jina lolote LIMEBEBA uumbaji wa kitu. Mfano: Kama ni gari jina la gari linabeba aina ya uumbaji wa hilo gari, kama ni mti unabeba uumbaji wa huo mti kupitia hilo jina, hivyo jina la kitu linabeba uumbaji.

Katika WANADAMU, kuna jina ambalo linabeba wanawake wote, kwa sababu huwezi kumuita mwanaume kwa jina la mwanamke; Kwa nini? Kwa sababu jina ndilo linabeba uumbaji na jinsia pia.

Mtumishi wa Mungu Mtume na Nabii, Josephat Elias Mwingira

Mungu alipomuumba Mtu, baada ya kumfanya kuwa tayari kwa kutumiwa aliumba wanyama. Akampelekea huyo Mtu ili awape majina; Naye Adamu aliwapa majina hao wanyama sawa sawa na uumbaji wake. Lazima uelewe kuwa jina linalenga uumbaji.

Mwanzo 5:1-2, “Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya; mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa”.

Adamu siyo Mwanaume au Mwanamke; Adamu ni nani? Adamu ni UUMBAJI, kwa kuwa Mungu alipowaumba aliwapa jina hilo.

Mfano:- Mtu akizaa mtoto wa kike ataitwa Binti wa fulani na kama ni wakiume ataitwa bin fulani. Hii inamaana gani? Inamaana kuwa jina linabeba TABIA ya Mtu, kila jina lina TABIA yake.

Mfano:- Watu wanaoitwa Josephat siku zote ni watenda kazi, na hawana hofu hawaogopi chochote na niwaongeaji.

Usimpe mtoto wako jina kama hujui linamaana gani, usimpe jina kwa sababu rafiki yako anajina ambalo unaona ni zuri unaweza kumsababishia matatizo. Chunguza kwanza jina linamaana gani ndipo umpe mwanao kwa sababu jina linabeba ubaadae wa Mtu.

Mwanzo 17:1-6 “Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana…. ”

Jina linabeba ubaadaye wako, kama Bwana anataka kubadilisha ubaadaye wako au kukufanya uwe mtu mkuu, lazima atabadilisha jina lako kwanza kabla ya kukutumia.
Jina linabeba ubaadaye wa mtu, je wewe unaujua ubaadaye wako? Jina lako linamaana gani? Wakati mwingine tunafikiria kuwa tuna majina mazuri lakini kumbe yana maana tofauti na ubaadaye wetu.

Wakati Mungu anataka kumfanya Abrahimu kuwa Baba wa Mataifa, aliangalia jina lake na kuona kuwa linamzuilia yeye kuwa kama alivyo mkusudia, ndipo akambadilisha kutoka kuitwa Abrahamu na kumuita Ibrahimu. Mungu alipotaka kumbariki Abrahamu hakumkemea shetani atoke bali alibadilisha jina lake.

Kwa mamlaka niliyo nayo, leo ninakutamkia kuwa kila jina linalo zuia ubaadaye wako ninaliharibu katika Jina la Yesu, naiwe hivyo.

 

UJUMBE : FANYA KAZI

Kama MUNGU alifanya kazi nawe pia ni lazima ufanye kazi. Kama unataka kustawi ni lazima ufanye kazi kwa bidii, amua weka mikakati fanya kazi na MUNGU atakubariki. Acha kukaa na kulalamika amka fanya maamuzi, wewe una kibali popote utakapo kua.

Uwe mtu wa kutatua changamoto za watu sio na wewe unalalamika maana wewe unamuwakilisha MUNGU aliye hai, mweza wa yote katika yote.

FANYA KAZI.

SOMO: NI JINSI GANI IMANI YETU INAWEZA KUJENGWA KATIKA FUNDISHO LAKE.

MTUME NA NABII: JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA

Tupo katika safari ya kujua sisi ni nani ndani yake (Mungu) kama Biblia inavyosema.
Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuomba sawa sawa na mafundisho yake, hakuwaambia waombe sawa sawa na mafundisho ya Musa bali ni sawa sawa na mafundisho yake yeye.
Ili uwe na nguvu katika imani yako ni lazima maombi yako yajengwe katika fundisho lake (Bwana Yesu).

Mathayo 6:9-10 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.”
Mpaka hapa Bwaa Yesu hakuwaambia wanafunzi wake nini cha kuomba kwa Mungu bali alikuwa anawasaidia ili wajue wao ni akina nani ndani ya Baba wa Mbinguni.

Wafuasi wa Musa walijifunza jinsi ya kuomba sawa sawa na mafundisho ya Musa, wana wa manabii walijifunza namna ya kuomba sawa sawa na mafundisho ya huyo nabii, wafuasi wa Yohana Mbatizaji walijifunza namna ya kuomba sawa sawa na mafundisho ya Yohana. Vivyo hivyo na wanafunzi wa Yesu walienda kwake na kumuomba awafundishe namna ya kuomba, kwa sababu waliona mafarisayo wakiomba. Kwa nini kuomba? Kwa sababu maombi ni namna ya mahusiano ya mtu na Mungu, au kati yako na yule unaye muamini, hivyo tunatakiwa kujifunza namna ya kuomba.

Baada ya wanafunzi wake kumuomba awafundishe jinsi ya kuomba Yesu akawajibu kwa majibu mazuri sana, hakusema wasiombe la! Bali alijua umuhimu wa kuomba. Akawaambia kwenu ninyi msiombe kama wao wanavyo omba, kwa sababu ninyi ni wafuasi wangu. Mathayo 6:9-10 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.”
Maombi siku zote yanamfuata kiongozi anaye kuongoza, je! Wewe kiongozi wako ni nani? Omba sawa sawa na uongozi ulioko juu yako, kwani unapo omba sawa sawa na uongozi huo unapewa dhawabu sawa sawa na uongozi huo.

kama uko chini ya Musa utapokea sawa sawa na Musa kama uko chini ya Ibrahimu pia utapokea kutoka kwake. Je! Wewe uko chini ya uongozi gani? Omba sawa sawa na huo uongozi, ili upokee dhawabu kutoka kwa huyo kiongzi anaye kuongoza.

MUNGU ANAHITAJI UMPE NAFASI NDANI YAKO

Ni sawa umeokoka unaujua UKUU wa MUNGU na UWEZO wake lakini bado hauonekani kwako kwa nini?.

Mfano: Mwanaume anapomchumbia msichana akitaka kuoa jambo la kwanza atamweleza msichana dhamira yake. Binti akisikia ataangalia kupitia maneno yake, akiona nafasi yake (kukubaliwa kupendwa) ndani ya huyo mwanaume na akijua umetambua uzuri/urembo wake na umuhimu wake atamkubali na atajiachia kwake.

Kadhalika MUNGU akiona unamwendea na akiona ndani ya MOYO wako unampa YEYE nafasi na sio mwingine anaingia na kukaa ndani yako, hapo ndipo utaziona NGUVU zake, BARAKA zake, REHEMA zake, UPONYAJI wake ndani yako. AMUA LEO KUMPA MUNGU NAFASI MAISHANI MWAKO ILI MUNGU AINGIE NDANI YAKO.

KAMA UNATAKA KUOKOKA LEO ANDIKA NAMBA YAKO YA SIMU NA MAHALI ULIPO, TUTAWASILIANA NAWE HARAKA. MUNGU AKUBARIKI.
Mtume na Nabii: Josephat Elias Mwingira

 

SIKILIZA MAHUBIRI IBADA YA JUMAPILI HII KUTOKA KWA MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA

SOMO : UBABA – MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA

Nimegundua watu wengu hapa duniani, asilimia 80% au 90% wanateseka kutokana na kukosa mapenzi ya Ubaba, Ubaba siyo uzazi, unaweza ukatengeneza mtoto kwa sababu una uwezo, Ubaba ni tofauti na uzazi.

Mafalisayo na wanafunzi wa Yohona Mbatizaji walikuwa wakizozana juu ya ni nani anajua kuomba, kwa kuwa Yohana alikuwa anawafundisha wanafunzi wake namna ya kuomba na mafalisayo pia walikuwa wanajua namna yao ya kuomba ndiyo maana hata walipo kwenda kwa Bwana Yesu akasema ninyi salini hivi Mathayo 6:9-10 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. ” na wala msisali kama wale wanavyo Sali. Kwa kuwa kwako wewe siyo Mungu tu bali ni Baba yako pia.

Bwana Yesu alikuwa anawafunza na kubadilisha mtazamo wao wa jinsi ya kuwaza, je wewe unawaza nini kumuhusu Mungu?

Yohana 1:12  “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; ” Yeyote anaye mwamini Bwana Yesu Mungu anamfanya kuwa mtoto wake. Pindi unapo omba na kumjua Bwana Yesu ni nani na Mungu ni nani kwako na ukaomba kwa mtazamo huu, kamwe hutawahi kuona kushindwa katika maisha yako. Maombi yako hayatawahi kukataliwa.

Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake juu ya kuomba.

 1. “Baba yetu uliye mbinguni” na siyo Mungu wetu uliye Minguni, aliwafundisha hivyo ili wapate kujua kuwa wanaye Baba Mbinguni, unapo omba jua kuwa unaye mwomba ni Baba yako ndipo maombi yako yatajibiwa.
 2. “Jina lako litukuze” lazima ulitukuze jina lake, usiombe tu ilimradi umeomba, bali kabla hujaomba au kufanya kitu chochote elewa kwanza mtizamo wako kwa juu ya kile unacho kiomba, kwani unapo omba Mungu anaangalia mtizamo wako kwanza kabla ya kusikiliza maombi yako.
 • Kabla hujamuomba Mungu kitu chochote mtukuze kwanza na umuoneshe heshima yake.
 • Eneo lolote ambalo wanajua namna ya kuheshimu wakubwa zao hata kuabudu wanajua pia, wale watu wasiyo elewa habari ya heshima kwa wakubwa zao wanapenda kuomba na siyo kuabudu. Mungu haangalii sana kuomba kwa mtu bali anaangalia ibada (kuabudu), unapo abudu ndipo Mungu anasikiliza maombi yako kwa haraka.
 • Bwana Yesu alikuwa anatufundisha heshima ya kwenda mbele za Mungu, maana kwa hali ya kawaida mtu akienda kwa baba yake huwa anaonyesha heshima kwanza kabla ya kuongea chochote, hivyo kwa Baba yetu wa Mbinguni ni zaidi ya hayo.
 • Bwana Yesu pia ametufundisha kuwa kabla hujaanza kuomba ni lazima ujue ninani unaye muomba, je! ni mjomba wako, kaka yako au nani kwako?. Kwa kadri unavyo muheshimu baba yako aliye kuzaa ndivyo hivyo hivyo utakavyo muheshimu Mungu, kama humuheshimu baba yako aliye kuzaa hutaweza kumuheshimu Mungu kwani hutaweza.

Kabla hujaomba itafute heshiuma ya baba yako wa mbinguni ili, Usimchukulie Mungu kama baba yako ukamuona ni mkosaji ukamjumlisha na Mungu.

 1. Ufalme wako uje; kile kinacho fanyika Mbinguni na hapa duniani pia kifanyike, inamaana kuwa alikuwa anaongelea kuhusu ufalme, mfano kwa hali ya kwaida Mfalme huwezi kumchezea maana anaweza kukuua, na ndiyo maana Bwana Yesu alikuwa anatufundisha jinsi ya kuomba, kwa maana unapokwenda mbele zake bila adabu atakumaliza au utatoka na laana.

Unapaswa kuwaheshimu Watumishi wa Mungu kwani ni Mungu Mwenyewe ameamuru hii, yeye amesema “usiseme masihi wangu”. Je wewe ni mara ngapi umekuwa unawasema watumishi wa Mungu vibaya? nimara ngapi wewe umewadharau viongozi wako? Halafu unataka Mungu akubariki, kwa namna gani? Unapaswa kuwa na heshima kwa wale wanao kuongoza ndipo utaweza kupokea Baraka kutoka kwa Mungu.

Inakuwaje mtu aliye okoka anapatwa na magonjwa  kivipi wakati wewe umemjua Mungu? wakristo wengi wanateseka kwa sababu ya kuto kutilia maananani mambo  ya Mungu, siyo mapenzi ya Mungu wewe uteseke, la! mapenzi Yake ni wewe uwe na afya njema.

 1. Mapenzi yake yatimizwe hapa duniani; Inamaana kuwa,
 2. Ubaba yeye yupo makini katika ubaba wake,
 3. Jina lake yeye yupo makini sana kuhusu jina lake, na ndiyo maana akasema usilitaje jina langu kama wewe si mtakatifu.
 4. Mapenzi yako yatimizwe; unatakiwa ujue Mungu anataka nini kwako

Kuna mambo mawili ninayapenda katika maisha yangu,

 1. Ninapenda kuabudu au waabudua maana Mungu anapenda wanao muabudu, ukitaka Mungu akutembelee anza kuabudu ya siyo kuomba
 2. Ukitaka kumsababisha Mungu akujie na kukutembelea usiku na mchana ni matoleo yako, mpe yeye
 3. Upendo; upendo ni nini? Ni kumfikili kumuwaza au kumtafakari yeye, un aweza ukawa na mahusiano na Mungu lakini haumpendi, Suleimani alikua na mapenzi sana na Mungu sawa na wimbo ulio Bora, hii ina maana gani? Nipokuwa nata kumuoa mke wangu Eliakunda….?

UJUMBE: Ubaba

Mathayo 6: 9-10 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.”

Bwana YESU Ametuambia kuwa tunapoomba tujue kuwa tunaye BABA, ukisali Sala hii inakuongoza jinsi gani ya KUOMBA.

Ukiwa na ile Roho ya UBABA unakuwa na NIDHAMU, ADABU na HAKUNA CHA KUKUSHINDA maana mwenye UBABA Hayumbishwi na Kitu chochote.

Mtu Anayejua kuwa anaye BABA hawezi kupotoshwa na mtu yeyote yule.

Mtu ambaye Amelelewa na wazazi wake wote wawili mara zote anakuwa na Adabu na Maisha yake yanakuwa ni ya Kustawi. Hii inakuwa tofauti kwa yule aliyelelewa na Mjomba, Shangazi au Bibi hana makazi maalumu, kwani Maisha yake yanakuwa ni ya tofauti na yule aliyelelewa na Baba na Mama kwa sababu alijifunza kwa kuangalia kile mama ama baba Wanatendeana.

Mtu ambaye hakulelewa na baba na mama hata maisha yake ya Ndoa yanakuwa ni ya shida maana hakuona Upendo ambao Baba na Mama yake walikuwa nao.

Mtu mwenye Roho ya UBABA Huwezi kumsukuma, akianza jambo Analimaliza maana HAJUI Kushindwa.

Yamkini kuna mambo yaliyokuwa yanakuonea, unasukumwa na kuonewa lakini sasa tumeelewa kuhusu UBABA, kama ni ndoa yako ilikuwa inasumbua TAMANI kupata ROHO HII YA UBABA ili ipate KUKUBADILISHIA Maisha yako maana UKIIPATA Hii hata ukianza Biashara ITAFANIKIWA.

Wale wenye UBABA wana TUMAINI, TEGEMEO na MSAADA hivyo huna Sababu ya Kushindwa, hata kama Ulizaliwa katika familia ya kichawi Ukipata ROHO YA UBABA UTAFANIKIWA kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu Baba yetu wa Imani.

HASARA za Mtu aliyekosa UBABA:-
• Anaonewa.
• Anadharauliwa.
• Anasukumwa na
• Kila anachokifanya hakiendi, na hata akioa au kuolewa mara nyingi huwa Wanaachana kwa sababu ya kukosa ROHO YA UBABA, au
• Akianza biashara inakufa.

Ukiipata ROHO HII YA UBABA Maisha yako YANABADILISHWA.

ROHO YA UBABA NI YA MUHIMU SANA KATIKA MAISHA YAKO.

MAMA ELIAKUNDA MWINGIRA. Efatha Ministry mwenge