Posts

UJUMBE ZIARA YA KITUME NA KINABII – MWANZA 3

SOMO: NGUVU YA MUNGU – MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA

Katika kumfanyia Mungu IBADA, uelewa wako ndiyo wa Muhimu zaidi kuliko ile Ibada unayoenda kufanya. Yaani mwendee Mungu wako huku ukielewa YEYE ni NANI na ANAWEZA Kukufanyia nini.

Mfano: Kaini na Habili walipomwendea Mungu Habili alimwendea huku akielewa yeye anaenda kufanya nini kwa Mungu wake na akielewa Mungu wake anaweza kumfanyia nini, na ndiyo maana Mungu akaifurahia sadaka yake.

UELEWA wako kwa Mungu wako kuwa YEYE ni NANI kwako na ANAWEZA nini, ndiyo Unaoweza kusababisha Maombi yako Kujibiwa.
– Unapokuja Kanisani SIKILIZA sana Unayoelekezwa ili uweze kumfanyia Mungu wako Ibada huku ukielewa YEYE Anaweza kukufanyia nini. (UELEWA wako ndiyo jambo la Msingi sana katika Ibada).

Bwana YESU aliwafundisha wanafunzi wake kuhusu Ibada, aliwaelekeza kuwa wao wasifanye Ibada kama wale wengine wafanyavyo, alikuwa anamaanisha kuwa wao wafanye Ibada kwa kuelewa kuwa yule wa Mbinguni ni BABA yao na ATAWAJIBU.

MAOMBI yoyote unayofanya hakikisha yanakuletea Mambo haya matatu; yaani AKILI KICHWANI, YESU MOYONI na PESA MFUKONI.

MTEMBEO WA MUNGU UMEAMBATANA NA MAMBO HAYA:
1. Upendo wa Mungu
2. Neema ya Bwana, hapa ndipo zimejaa huruma na fadhili zake.
3. Nguvu ya Mungu, Mungu hutembea na nguvu zake ili kudhihirisha mamlaka yake, Nguvu ni uwezesho wa kusababisha kitu kingine kiweze kufanya utendaji wake.
Kazi kubwa ya nguvu ni kuwezesha kitu au mtu kutenda kile ambacho kinatakiwa kutendeka.
Nguvu ya Mungu ndiyo inauweza wote, Mungu ndiye asili ya nguvu zote. Mfano: Hata ukitengeneza spika, kule ndani kuna madini yaani magnet, lakini asili ya zile magnet ni Mungu maana yeye aliviumba tangu mwanzo.

Nguvu ya Mungu imegawanyika katika sehemu kuu mbili;
1. Nguvu za uharibifu: Zipo pale kwa ajili ya kuharibu na uharibifu.
2. Nguvu za Baraka: Hizi zipo kwa ajili ya wema, na hutusaidia sisi kufanikisha mambo yetu.

Nguvu hizi mbili zinaweza kufanya kazi kwako kwa jinsi utakavyo amua au kuchagua, ukiamua kutenda mambo ya wema basi nguvu ya Baraka itaambatana na wewe lakini ukiamua kutenda mambo ya uovu jua kuwa nguvu ya uovu itaambatana na wewe.
Mungu ameziweka hizi nguvu mbili na kumuwekea mwanadamu maamuzi ya kuchagua ni nguvu ipi atembee nayo. Mungu hamchagulii mtu ila maamuzi yako ndiyo yatakayo mfanya yeye akupe. Je! Wewe maamuzi yako ni yapi? Unataka kutembea katika nguvu ipi, maamuzi yako ndiyo yatakayo amua ni nguvu ipi utembee nayo, amua kutembea katika mema ili nguvu ya wema na Baraka iambatane na wewe.

UJUMBE ZIARA YA KITUME NA KINABII – MWANZA 1

SOMO: UBABA NA UWANA; MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA.

Mathayo 11:25 “Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.”

Kuna mambo ya Mungu ambayo Amewaficha watu wenye Hekima, na kuwafunulia wale Waliokusudiwa.

Akili ya kibinadamu haitakaa ikufunulie siri za Mungu kwa sababu Kuna mengine wachache ndiyo wanafunuliwa; mfano: Elimu ya kuishi, huwezi kujua huyu atakuwaje baada ya muda gani, au atakufa lini bali BABA wa Mbinguni na MWANA ndiyo wanayo siri hiyo. Ili uyajue yale ambayo wachache wamefunuliwa lazima MWANA akufunulie.

UFUNUO WA UBABA NA UWANA UNAUPATAJE?
Yohana 17:5 “Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.”

Ufunuo wa UBABA na UWANA unapatikana katika; JINA la KRISTO na Neno lake.

Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa Neno la Kristo.”

Hivyo ili ujue uhalisia lazima umsikilize yule ambaye amepewa JINA.

– Neno litakupa KUFAHAMU Uhalisia kuhusu huyu BABA wa Mbinguni.
– Ili umjue Mungu ambaye ni BABA lazima ukutane na mtu ambaye analijua Neno, na amefunuliwa siri hiyo na Mwana (Yesu) ndipo atakujuza nawe siri hiyo.

Ukimwamini BWANA YESU, MUNGU wa Mbinguni anakufanya kuwa MWANAE.

Yeyote Atakayemkubali na Kumpokea Bwana YESU, mtu huyo anao UZIMA wa Milele, na Mungu aliyeumba Mbingu na Nchi anampa KIBALI cha kuwa MWANA WAKE.

Wewe kuwa MWANAYE hasemi UTUBU dhambi zako au uhakikishe kuwa wewe ni MTAKATIFU sana, anataka UAMINI tu kuwa YESU KRISTO ni BWANA.

Dhambi zako haziwezi kufutika ukitubu kuanzia asubuhi hadi jioni, zinafutika pale UKIAMINI kuwa HUYO unayemwendea ana Uwezo wa Kukusafisha au Kukutakasa. Je! wewe UNAAMINI?

Ili uweze KUSAMEHEWA ni lazima UAMINI, ukiamini kuwa YEYE ANASAMEHE makosa Muendee, lakini ukiamini kuwa ANAHUKUMU dhambi usimuendee maana ATAKUHUKUMU.

Mimi nina Amini kuwa nikienda mbele zake YEYE Ananisamehe dhambi zangu, kwa jinsi utakavyo Amini ndivyo itakavyo kuwa kwako.

Je! wewe una AMINI nini?

Wakati wa kina Petro walipomkuta yule kiwete ambaye alikuwa anaombaomba, akawaomba na kudhani kuwa watampa fedha lakini wa kina Petro wakamwambia kuwa sisi hatuna fedha wala dhahabu ila tulichonacho ndicho tutakupa, wakamwambia “ kwa JINA LA YESU inuka na uende”, yule mtu ALISIMAMA na KUTEMBEA.

Baada ya Wayahudi kusikia hayo, wakawaita wakina Petro na kuwauliza “NI KWA NGUVU GANI NA KWA JINA LA NANI, MMEFANYA HIVYO? Kuna mambo mengine ili uyafanye ni lazima uwe na JINA na NGUVU ndiyo Unaweza kufanya na siyo kwa Elimu.

Ufunuo wa Mungu katika JINA LAKE na NENO LAKE, na ili ufikie Kufahamu ile siri, sehemu ya Kwanza ni lazima ujue Mungu amekuandalia nini wewe, usiogope katika chochote alichokuandalia pita hapo hata kama ni matusi au mateso pita maana ukimaliza UTATUKUZWA.

1 Yohana 3:1 “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.”

KAZI YA PENDO LA MUNGU:
a) Ukilipata PENDO la Mungu litashughulikia mahitaji yako; mfano: Ule nini, Uvae nini, n.k. Mathayo 6:34 “Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”

  1. b) PENDO la Mungu, Linakuhakikishia Uwana; yaani kwamba wewe ni MWANA wa Mungu.
  2. c) Linakupa KUSHUHUDIA wengine na kufanyika USHUHUDA kwa wengine, maana linakuumbia UJASIRI.

Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

Mungu anaposema utafuteni kwanza UFALME wake, hazungumzi na ambao hawajaokoka bali wale ambao tayari Wameokoka, na Wanamjua Mungu.

– Hamu yako ya KUMTAFUTA ndiyo Humfanya YEYE akuonyeshe UZURI wake. (Ukimpata na Ukilipata PENDO lake, swala la wewe Uvae nini au Ule nini linakwisha).

UTAFUTE KWANZA UFALME WAKE NA HAKI YAKE HAYO MENGINE YATAKUJA KAMA ZAWADI TU KWAKO.

Kanisa la YESU KRISTO halitakaa liwe na Nguvu kama halina MAFUNDISHO, na halitakaa lichukue Nafasi yake iliyokusudiwa kama hawajafundishika, kwa kadri utakavyokuwa tayari KUFUNDISHWA nawe Ukafundishika ndivyo utakavyoweza kufika kule ambapo Mungu AMEKUKUSUDIA.

UPENDO WA MUNGU:
Pendo la Mungu linamaanisha UUMBAJI wa Mungu, Mungu aliumba vitu vyote na AKAVIPENDA. Mwanzo 1:31 “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.”

UUMBAJI woote Umeumbwa katika Pendo la Mungu, hivyo ili uweze kufanya uumbaji wa kitu chochote ni lazima uwe na Upendo, huwezi kubuni kitu chochote kama huna UPENDO. Mfano:- Ili uwe mkulima mzuri na upate mazao ni lazima upende kilimo, pia ili uweze kufuga ni lazima upende wanyama, ukiona unafuga wanyama na wanakufa jua kuwa hauna Upendo.

Huwezi kusababisha watu Waokoke kama hupendi wenye dhambi, kama huwapendi usitarajie kuwa Kanisani kwako watakuja watu, maana siku hizi Watakatifu ni wachache sana.

Pendo ndilo linalosababisha uwe na kitu, huwezi kufanya biashara kama hupendi kuongea na watu.

Ukiweza kupenda au ukiwa na Roho ya Kupenda kilichoumbwa na Mungu, iwe ni miti, majani, watu au vitu ukivipenda basi wewe ni rahisi kuikamilisha siku yako iwe njema, kama huwezi kuvipenda kamwe hutaweza kuikamilisha siku yako. Maana ili uishi ni lazima uvipende vilivyoumbwa na Mungu.

UJUMBE ZIARA MKOANI MARA (SEHEMU YA PILI)

SOMO : UBABA – MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWIGIRA

Mathayo 11:25-27 “Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, ..…”
Nani amefunuliwa?
Yesu yeye ndiye wakwanza kabisa kufunuliwa na Bwana na akaja kwetu kwa kupitia Mariamu ili awe mwanadamu kama sisi, akala, akalala na akachoka kama mwanadamu lakini hakufanya dhambi, hii ndiyo ya kushangaza sana. Bwana Yesu hakufanya dhambi kwa sababu hakuzaliwa katika nguvu ya dhambi.
Nguvu ya dhambi inatokana na kosa la Adam lakini yeye hakupitia huko maana hakuzaliwa kwa namna ya kibinadamu bali kwa namna ya ki-Ungu hivyo nguvu ya kufanya dhambi kwake haikuwepo. Lakini yeyote aliyezaliwa kwa njia ya kibinadamu yaani aliyezaliwa na Baba na Mama kunakuwa na nguvu ya mvutano ambayo bila nguvu ya Mungu nguvu hiyo ya dhambi itampelekea yeye kufanya dhambi.
Mwanzo 3: “Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele;”
Ndani ya mwili wa mwanadamu kuna nguvu za aina mbili:-
a. Nguvu ya kujua mema na
b. Nguvu ya kujua mabaya
Kuna saa nguvu ya mema inamsukuma mtu ili afanye mazuri, saa nyingine nguvu ya mabaya inamsukuma na kujikuta nafanya mabaya (dhambi). Sasa inategemea kwa wakati huo ni nguvu ipi inayo tenda kazi. Inakupasa kuwa makini kujua je! Ni nguvu ipi ambayo wewe unatembe nayo na kufanyanayo kazi? Unapaswa kutembea na Nguvu ya Mungu wakati wote.

Siku za mwanzo unapomtafuta MUNGU unaonekana kama hufai kabisa, lakini unapomuona SHANGWE inaonekana kwako. Ukikutana na maono ya Mungu kuna MABADILIKO yanatokea katika maisha yako. Kama MWANA (Bwana Yesu) hajakujaalia au kukufunulia kumuona au kumjua Mungu hutakaa umuone; Maana uweza huo umewekwa kwake yeye tu.

Zaburi 16:11 “Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.”

Unapoijua njia ya Bwana unajawa na FURAHA na AMANI ya Bwana milele; Hivyo Ustawi kwako ni lazima, ukishapita kwenye ile njia hakuna tena kujuta kuna kushangilia, kuna Amani na furaha ya milele. Ukimuona mtu aliye okoka anajutia wokovu wake basi ujue huyo hajaokoka, kwa sababu mtu yeyote aliye okoka sawa sawa anakuwa na mabadiliko.

Mtu anapo okoka Mungu anaangalia kile kinachomfanya huyo mtu akose furaha ndiyo anakiondoa kwanza ili USIJUTIE wokovu aliyokupa; Akiona unaendelea na wokovu anaondoa kimoja baada ya kingine kile ambacho kitakuondolea furaha ya wokovu wako mpaka vyote viishe na ndipo unafika mahali pa kuelea katika Utukufu wake.

Ukifika mahali ukakutana naye utasema NIMEMUONA MWANAUME, Yesu akitokeza katika maisha yako kila kitu kilichopinda kinakaa katika mstari wake; Maana mkononi mwake mnamema ya milele.

Huwezi kufikia toba ya kweli kama hujakutana na mwokozi wako, mtu aliyeokoka akisikia Neno linahubiriwa iwe lina muhusu au halimuhusu hasemi hili si la kwangu ni la fulani, bali ANAJITATHMINI mwenyewe na kuona kuwa AMEKOSEA ANAJIREKEBISHA au kama yuko sawa anamshukuru Mungu. Mtu aliyekombolewa huwa ANAJITENGENEZA ili azidi kuwa bora, lakini wale ambao hawajakombolewa pindi anaposikia Neno anasema hili siyo langu bali ni lafulani, kama wewe ni mmoja wao jua kuwa hujakombolewa bado, jitahidi ili ufikie katika TOBA YA KWELI. Mtu aliyekutana na Yesu huwa anasema ya kwake na Mungu wake na si ya watu wengine.

Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani. Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri,” 
Daudi alikuwa hasemi ya wenzake bali alikuwa anasema ya kwake ili apate KUKOMBOLEWA, Mungu anapendezwa na KWELI ya mtu iliyo MOYONI mwake.

Laana ikikushambulia, Unaishi kwa mashaka na hata kufa unakufa kabla ya wakati wako kufika. SIYO RATIBA ya Mungu wewe ufe mapema, bali Ratiba yake ni wewe UISHI mpaka muda ule aliokusudia YEYE ufike; Sio RATIBA YA MUNGU wewe Uishi kwa MASHAKA au DHIKI, Ratiba yake ni wewe uishi kwa KUCHANUA hapa chini ya jua.

Zaburi 109:14-16 “Uovu wa baba zake ukumbukwe mbele za BWANA, Na dhambi ya mamaye isifutwe. Ziwe mbele za BWANA daima, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. Kwa kuwa hakukumbuka kutenda fadhili, Bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, Hata akamfisha mtu aliyevunjika moyo,”

Baba yako akifanya dhambi ASIPOTUBU inakumbukwa kwako na unadaiwa, kila wakati ibilisi ANAKUSHITAKI kwa Baba wa Mbinguni na anakushinda. Hata UNAPOOMBA mbele za Mungu hakuna KINACHOTOKEA kwako, unafunga usiku na mchana na hakuna kinachotokea.

Zaburi 109:6-8“Uweke mtu mkorofi juu yake, Mshitaki asimame mkono wake wa kuume. Katika kuhukumiwa ataonekana hana haki, Na sala yake itadhaniwa kuwa ni dhambi. Siku zake na ziwe chache, Usimamizi wake na atwae mtu mwingine.”

Utajuaje Mkono wa Mungu uko juu yako? Utaona kila kitu au mtu anayeinuka kinyume chako ANASHINDWA. Zaburi 89:20-23 “Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu. Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu. Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa.” BWANA akikupaka mafuta anakutia NGUVU na FADHILI zake zinakuzunguka na yule anayekuonea ANAONDOLEWA kwako.

OMBI: Ee BWANA kama liko jambo lolote linalonikandamiza au kunirudisha nyuma naomba uliondoe leo katika maisha yangu.

 

UJUMBE ZIARA – MARA (SEHEMU YA KWANZA)

SOMO: UBABA – MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA.

Mathayo 11: 25, “Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia”.

UBABA ni tofauti na kuwa mzazi, UBABA ni ROHO au TABIA; Bwana Yesu akasema nakushukuru Baba, Bwana wa Mbingu na Nchi kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili ukawafunulia watoto wachanga.

UBABA ndio wenye kufunua SIRI; Unatangaza UBADAE wa Mtu na UNAFUNUA mambo yaliyofichika. Mfano kabla mtu hajafa ubaba unafunua siri ndio maana mtu anasema shamba hili ni la mtu fulani, nyumba hii niya fulani, wewe ulijua ni yakwako kumbe ana siri moyoni mwake.

Huyu Baba ambaye nataka ujue habari zake ni Bwana wa Mbingu na nchi. Kuna watu wana akili na hekima na ni Mungu mwenyewe amewapa ila kuna mambo amewaficha na amewafunulia watoto wachanga. Anaposema watoto wachanga anamaanisha watu ambao ni wanyonge, wasio na majina, wasio tambulika na wasio pewa heshima, hao ndio anao wafunulia.

“Kumfahamu Mungu inatokana na mapenzi yake maana yeye ndiye anaye kufunulia”.

Unaweza kutembea hapa duniani mpaka ukafa pasipo kumjua Mungu, unaweza kwenda kanisani miaka mingi na ukawa humjui Mungu. Kuna watu wanafundisha kwenye masinagogi lakini hawamjui Mungu, ndio maana hawakuweza kukusaidia mpaka ulipokuja kwa wanaomjua Mungu wakakusaidia ukafunguliwa.

Mathayo 11: 27, “Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia”.

Yesu akasema nimekabidhiwa vyote na Baba yangu wala hakuna amjuaye mwana ila Baba na hakuna anayemjua Baba ila MWANA. Mwana ndiye aliyepewa KIBALI cha kutambulisha.

Mifano kutoka katika BIBLIA

  1. Adamu alikuja kudhihirisha kwamba Mungu ni MUUMBAJI ndio maana baada ya MUNGU kuumba wanyama walipelekwa kwa Adamu akawapa majina.
  2. Nuhu alikuja kutambulisha anayeweza kuangamiza, anayeweza kutoa na kuurudisha uhai. Alifundishwa namna ya kuokoa uhai, yeye pekee ndiye alifundishwa kutengeneza wokovu kwa vitu vilivyoumbwa. Ndiye mtu wa kwanza aliyefundishwa namna ya kuokoa, Adamu hakufundishwa hivyo.
  3. Ibrahimu alifundishwa ili uweze kuokolewa lazima uwe na Imani kuhusu Mungu, akasimama na akaokoa jamii kubwa kwa imani.
  4. Musa alifundishwa namna ya kumjua Mungu kwa njia ya sheria; Unajulikana wewe niwa Mungu kwa matendo yako.
  5. Samweli na wenzake walijifunza kumjua Mungu katika Neno, ujumbe ukimjia ndio anajua Mungu anasema. Walifundishwa kumjua Mungu katika Neno.

Yesu alikuja kumtambulisha nani? Musa alimtambulisha Mungu kama Muhukumu au jaji, manabii walimtambulisha Mungu kama mwenye Neno wakasema Mungu wetu ni MOTO ULAO. Yesu anamtambua Mungu kama Baba; Huwezi kumfahamu mpaka Mwana akujalie huo UFUNUO.

Kama humjui MWANA huwezi kumjua Baba. Hutakaa umjue Mungu kama humjui Yesu na huwezi kumjua Mungu kama Yesu hajakufunulia. Lengo la Mungu kumtuma Yesu duniani ni ili sisi tuweze kutambua nafasi ya BABA wa Mbinguni katika maisha yetu.

Wakati huu Mungu anasema nasi kwa njia ya MWANA; Hutakaa UMJUE Mungu kama humjui YESU, na huwezi kumjua YESU kama Hajakufunulia.

YESU alikuja kwetu KUMTAMBULISHA Mungu mzima mzima, hakuja kumtambulisha kama Muumbaji, BWANA wa Mabwana, Muhukumu au Mfalme wa wafalme bali amekuja kumtambulisha kwetu kama BABA. Watu wengine kwao ni Mungu MUUMBAJI, MHUKUMU wa HAKI, MFAMLE wa Wafalme, lakini kwangu mimi ni BABA.

Mfano: Watu wanamuita Raisi wa Nchi Amiri Jeshi Mkuu, wengine wanamuita Mwenyekiti wao, wengine shemeji, wengine mjomba na kadhalika; Lakini mtoto wake anamuita BABA, anaweza kucheza nae akamrukia, akitaka kwenda Ikulu hahitaji kibali anaenda kwa Baba yake na haombi ruhusa.

YESU amekuja kuwatambulisha kuwa huyu Mungu mnayemuita MUUMBAJI, BWANA wa Mabwana ni BABA yako. Hata kama ulirogwa na shangazi yako, wachawi wakakufanyia walichofanya huyu BABA Atakusafisha.

Ndipo YESU akasema BABA nakushukuru kwa kuwa haya mambo uliwaficha wenye hekima na akili ukawafunulia watoto wachanga, kwa lugha nyingine anamaanisha ili uweze KUELEWA haya mambo lazima UKUBALI kuwa kama MTOTO MCHANGA.

Safari hii utauona UPENDO wa BABA yako, haijalishi tutahubiri kiasi gani unachotakiwa kujua yupo Mungu ambaye ni BABA yako na wewe ni MTOTO wake unataka Kumuona. Haijalishi ulizaa na mganga wa kienyeji au ulifanya dhambi gani mwambie YESU wewe unaelewa yote niliyopitia unirehemu.

YESU alikuja kukuonyesha Mungu Muumba wa Mbingu na nchi ni BABA YAKO na sio baba wa kambo; Na safari hii utamuona AKIKUPIGANIA.

Mathayo 11:25-27 “Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.”

Baba hana mpango wa kumfunulia mtu mambo yake bali amekwisha kumpa mwanaye Yesu ili awafunulie wale wanao taka kumjua Baba, na kujua anayoyataka kwao ni yapi, na yeyote ambaye mwana apenda kumfunulia basi humfunulia.

“Mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga” Anapozungumzia watoto wa chaga hazungumzii wale wanao nyonya, bali anazungumzia wale watu ambao hawajui mambo ya Mungu na wanataka Mungu awajulishe zaidi, hao wanakuwa ni wachanga kiroho na hao ndiyo Yesu anakwenda kujifunua kwao ili kuwajulisha zaidi kumuhusu BABA wa Mbinguni. Wewe usiwe kati ya wale waliyo fichwa bali uwe kati ya wale walio funuliwa, yaani usiwe mjuaji kwa mambo ya Mungu tamani yeye akufundishe kila iitwapo leo.

MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA KITUME NA KINABII – TEMEKE DSM

MATUJIO katika picha ziara ya Kitume na Kinabii Mkoa waTemeke ambapo Mtume na nabii na timu ya Mitume na waimbaji wa mass choir walitembelea kanisa la Efatha Kigamboni na Temeke lililopo mbagala.

 

UJUMBE: ZIARA YA KITUME NA KINABII, EFATHA MINISTRY – KIGAMBONI

MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA

Unakuta mtu anatumia pesa nyingi sana katika mahitaji yake ya kila siku lakini hampi Mungu chochote kile na anatarajia kuponywa.Mungu anaweza akakuhurumia na akakuponya, basi na wewe kuanzia saa hiyo anza kumuonyesha unamuheshimu kwa kutoa muda wako na mali zako kwa ajili yake.
Ukisoma katika Biblia kuanzia Mwanzo hadi Ufunuo utaona kuwa wale ambao waliponywa magonywa makubwa ni wale ambao walitoa mali zao, kazi zao na akili zao kwa dhati kwa Mungu
Watu wengi sana siku hizi wanataka kupokea kutoka kwa Mungu lakini hawataki kutoa chochote kwa Mungu.
Mungu alimtoa mwanaye mpendwa Yesu Kristo ili afe kwa ajili yako, lakini wewe unapokea uponyaji leo au unaomba na yeye anakujibu na anapokujibu huonyeshi shukrani yeyote kwake, SHUKRANI KWA MUNGU INAMFANYA AENDELEE KUKUBARIKI.

Kuna neno ambalo Mungu alimruhusu Bwana Yesu atufundishe sisi kuhusu Sara ya Bwana.
Mathayo 6:9-13 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni…” Alitanguliza mambo yanayo muhusu Mungu, Bwana Yesu anatufundisha kuwa usianze kuomba mahitaji yako kwanza kabla ya kujua kuwa Yeye anataka nini.
Katika maisha yako jifunze kumtukuza Bwana, fanya jambo ili Yeye aone na si wanadamu, waza na ongea mahali ambapo Yeye anatukuzwa, na watu ambao utashirikiana nao wawe ni wale wanaomtukuza Yeye.
“Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe,” Ufalme una kodi hivyo lazima uwe tayari kulipa kodi, yaani inamaana kuwa unapo ualika huo ufalme uje na wewe uwe tayari kuutumikia huo ufalme.

Mathayo 15:21-28 “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo……” Bwana Yesu anasema kuwa ametumwa kwa wale walio kusudiwa na wewe ni mmoja wao.
Ni ratiba ya Mungu kuponya hata wale wasio pendeka na ni mpango wake kuwahurumia hata wale wasio muita Yesu ni Bwana lakini wakitamani kuguswa na yeye anawaponya.

Mathayo 9:20-21 “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.” 
Ni mapenzi ya Mungu kuondoa misiba yote kwa wanadamu.
Tatizo hilo la kutokwa na damu lili mfanya yule mwanamke akose mambo mengi na likampelekea kuishi katika maumivu na mateso ya kila namna.
• Hilo tatizo lilimpelekea kuwa muhitaji kwani pesa alizokuwa nazo alitumia kujitibia.
• Alikuwa mpweke, alikuwa ni mpweke kwa maana hakuweza kuolewa, na hivyo akawa anaishi katika utasa.

Misiba, mateso na magonjwa mengi ambayo wanayo pitia wanadamu yanawafanya wawe masikini, kwani baada ya kwenda mbele wanarudi nyuma, kwani wanakusanya mali nyingi sana lakini inaishia katika kutibu magonjwa au kutatua matatizo.
Ni mara ngapi umekuwa kila ukipata pesa tatio linatokea? Siyo mpango wa Mungu kukupa pesa ili utibie magonjwa au utatue matatizo.
Mungu haleti pesa kwa ajili ya majanga bali ni ili wewe Uchanue na Kustawi.

Yeremia 32:27 “Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?” Hakuna jambo gumu kwa Mungu yote yanawezekana kwake.

MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA KITUME NA KINABII – ILALA

Matukio katika Picha: Mtumishi wa Mungu Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira alipotembelea na kufungua Kanisa la Efatha Ministry Matunda na Ushindi, Mazizini na maeneo mengine.

 

UJUMBE ZIARA YA KITUME NA KINABII MKOA WA ILALA DSM

MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA.

Mungu ni Mungu wa wote wenye mwili, unaweza ukatengeneza mdoli ukamuita mungu wako, au ukaweka dhahabu ukatengeneza kitu ili ukiabudu au ukafanya meengi ya kukupendeza, lakini Baba wa Mbinguni atabaki kuwa Mungu wako milele.

Yesu hana dini bali ana WOKOVU, kwa vile hana dini anapokea kila mtu anaye mjia, anaangalia moyo uliyo tayari kutubu na kufanya mapenzi yake ili afanye makazi yake hapo.
Bwana Yesu amekwisha kutoka msalabani, anakaa ndani ya watu ili kubadiisha maisha yao, kama bado hujampokea MRUHUSU AKAE NDANI YAKO ILI ABADILISHE MAISHA YAKO

Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”
Chochote unacho kifanya hapa chini ya jua unapaswa kutambua kuwa “Neno la Mungu ndiyo taa” maana yake ni kuwa ukimjua Mungu hutakuwa maumivu kwa wengine bali utakuwa Baraka kwao.
Lifanye Neno la Mungu liwe taa ya miguu yako likumulikie ubaadaye wako, kazi zako na maisha yako na ili likuongoze na kukufanya kuwa Baraka kwa watu.
Neno la Mungu likikumulikia utaweza kuuona ubaadaye wako na litakupa kujua ufanye nini ili usiwe masikini bali uwe na pesa.
Kila mtu hapa chini ya jua Mungu amemuandalia kitu cha kufanya ukifanya cha mwenzako hutafanikiwa. Ili uweze kukijua kile ambacho Mungu amekuandalia kukifanya lifanye neno lake kuwa taa ya miguu yako litakuongoza pale ambapo unapaswa kuwa.