UJUMBE : SALA YA BWANA

UJUMBE SALA YA BWANA (Ibada ya Jumapili Oktoba 22 – 2017)

MTUME NA NABII: JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA

Wakati mwingine watu wanalichukulia PENDO LA MUNGU kama la mzaa mzaa, na huwezi kujua uzuri wa kitu mpaka umekipoteza. Katika Nchi yetu tuna Mungu mzuri ambaye anatujali na kutupa mambo yote tunayohitaji, lakini tunachukulia mzaa mzaa, mahali popote palipo na mkono wa Mungu panamsahama.

Mkono wa Mungu upo ndio maana hata watu wakifanyiwa uovu wanasamehe, pasio mkono wa Mungu hakuna kusameheana. Watumishi wa Mungu wanaomba usiku na mchana ili Mkono wa Mungu usiondoke kwetu na rehema zake. Katika nchi hii pekee unaweza kwenda kwa rafiki yako ukalala na kula usiulizwe lolote na unaweza kuoa kabila lolote, lakini majirani zetu yaani nchi zinazotuzunguka hawawezi kufanya hivyo, huwezi kula kwa mtu wala kuoa kabila lingine kwa urahisi, kwani kila kabila lina tabia zao na kushirikiana wao kwa wao.

Sisi watanzania hatuna hilo, Mungu ametupa Amani na Upendo. Unaenda kila mahali bila kuzuiliwa, ni katika nchi hii tu kuna Amani ya kumwabudu Mungu, na ni vizuri ukamwabudu Mungu sasa kwani kuna Amani ya kutosha, huwezi kumwabudu Mungu kama kuna vita na njaa. Mungu ametupa Amani ili tumwabudu sawa sawa na kuzionyesha nchi nyingine namna ya kuabudu katika roho na kweli.

Mimi nimezunguka katika nchi nyingi lakini sijaona nchi wanayoabudu kama Tanzania, sisi tunakorasi zetu na tuna nyimbo zetu tofauti na nchi nyingine kwani hatumwabudu Mungu ili atuondolee vita, atupe chakula au fedha, ila tunamwabudu kwa sababu Yeye ni Baba yetu na Muumbaji wetu.

Watu wengi wanaenda Kanisani wakiwa na mateso, magonjwa na maumivu ili Mungu ashughulike nao, usiende kwa Mungu namna hiyo bali mwabudu Mungu wakati kila kitu kina utulivu, mwonyeshe kuwa unampenda, tena usimwabudu kwa kuwa unataka kitu kwake usifanye hivyo. Mwabudu Mungu kwa sababu amekwisha kufanya jambo kwako.

Kuna watu hawawezi kwa sababu ya magonjwa na wengine wamekufa ila wewe upo hai, wengine ni vipofu lakini wewe unaona, wengine ni viziwi hawasikii, hawawezi kuongea kwa kuwa ni bubu, lakini wewe unaweza kuona, kusikia na kuongea kwa sababu hiyo mwabudu Mungu. Wengine hawana miguu lakini wewe una miguu na mikono unaweza kutembea mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yako kwa sababu hiyo unatakiwa umwabudu Mungu.

Wengine hawana hata nguo za kuvaa lakini wewe unazo nyingi za kubadilisha, wengine hawana chakula wewe unabadilisha leo ule wali, kesho ugali, chai na viazi, unachagua ule nini, kwa sababu hiyo unatakiwa umwabudu Yeye.

Kwa nini unasubiri mtu akusukume na kukuhamasisha kuabudu? Usisubiri wakati matatizo yatakapokuja ndio uanze kumwabudu hapana, mtafute Mungu na umwabudu sasa ili wakati matatizo yatakapo kuja Yeye awe ulinzi wako na ng’ome yako.

Mwabudu Mungu wakati unauwezo wa kuchagua, watu wanasubiri kumwabudu Mungu wakati hawana uwezo wa kuchagua kati ya mambo yao na Mungu. Mungu mwenyewe anasema alituchagua sisi, inamaana alikuwa na vitu vingi vya kuchagua lakini akatuchagua sisi, hata akamtoa mwanawe wa pekee aje afe kwa ajili yetu.

Kama unataka maisha amua kuwa na Yesu ili maradhi yakija awe Mponyaji na Mkombozi wako, chochote kikija kinyume chako awe Mwokozi wako, ni vema ukachagua kumwabudu Mungu sasa.

Mathayo 6:9-13 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] “

Kwa nini inatakiwa Ufalme wa Mungu uje juu ya maisha yako? Kwa sababu bila Yeye hatuwezi kufanya jambo lolote, ndio maana anasema Ufalme wake uje, Ufalme wake unapokuja katika maisha yako, kazi yako na familia yako nini kinatokea? Ufalme una namna yake ya kujiendesha na taratibu zake za kufanya mambo. Yesu akasema kwa ninyi waamini, wafuasi na wanafunzi mnatakiwa kuruhusu Ufalme wake uje juu ya maisha yenu, unatakiwa kuelewa kuwa pasipo yeye haiwezekani kufanya jambo lolote.

Katika Ufalme kuna waamini, wafuasi na wanafunzi makundi haya matatu yana utukufu wake na kila kundi lina Nguvu, Neema, Rehema za Mungu na Pendo la Mungu.

Waumini wanatakiwa kufundishwa sio kuombewa, wanapofundishwa wanajawa na Ufahamu wa Neno la Mungu na wanajua wako katika kundi gani na wanaweza kuchochea udhihirisho wa Roho Mtakatifu

Comments

comments

Comments are closed.