UJUMBE ZIARA MKOANI MARA (SEHEMU YA PILI)

SOMO : UBABA – MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWIGIRA

Mathayo 11:25-27 “Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, ..…”
Nani amefunuliwa?
Yesu yeye ndiye wakwanza kabisa kufunuliwa na Bwana na akaja kwetu kwa kupitia Mariamu ili awe mwanadamu kama sisi, akala, akalala na akachoka kama mwanadamu lakini hakufanya dhambi, hii ndiyo ya kushangaza sana. Bwana Yesu hakufanya dhambi kwa sababu hakuzaliwa katika nguvu ya dhambi.
Nguvu ya dhambi inatokana na kosa la Adam lakini yeye hakupitia huko maana hakuzaliwa kwa namna ya kibinadamu bali kwa namna ya ki-Ungu hivyo nguvu ya kufanya dhambi kwake haikuwepo. Lakini yeyote aliyezaliwa kwa njia ya kibinadamu yaani aliyezaliwa na Baba na Mama kunakuwa na nguvu ya mvutano ambayo bila nguvu ya Mungu nguvu hiyo ya dhambi itampelekea yeye kufanya dhambi.
Mwanzo 3: “Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele;”
Ndani ya mwili wa mwanadamu kuna nguvu za aina mbili:-
a. Nguvu ya kujua mema na
b. Nguvu ya kujua mabaya
Kuna saa nguvu ya mema inamsukuma mtu ili afanye mazuri, saa nyingine nguvu ya mabaya inamsukuma na kujikuta nafanya mabaya (dhambi). Sasa inategemea kwa wakati huo ni nguvu ipi inayo tenda kazi. Inakupasa kuwa makini kujua je! Ni nguvu ipi ambayo wewe unatembe nayo na kufanyanayo kazi? Unapaswa kutembea na Nguvu ya Mungu wakati wote.

Siku za mwanzo unapomtafuta MUNGU unaonekana kama hufai kabisa, lakini unapomuona SHANGWE inaonekana kwako. Ukikutana na maono ya Mungu kuna MABADILIKO yanatokea katika maisha yako. Kama MWANA (Bwana Yesu) hajakujaalia au kukufunulia kumuona au kumjua Mungu hutakaa umuone; Maana uweza huo umewekwa kwake yeye tu.

Zaburi 16:11 “Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.”

Unapoijua njia ya Bwana unajawa na FURAHA na AMANI ya Bwana milele; Hivyo Ustawi kwako ni lazima, ukishapita kwenye ile njia hakuna tena kujuta kuna kushangilia, kuna Amani na furaha ya milele. Ukimuona mtu aliye okoka anajutia wokovu wake basi ujue huyo hajaokoka, kwa sababu mtu yeyote aliye okoka sawa sawa anakuwa na mabadiliko.

Mtu anapo okoka Mungu anaangalia kile kinachomfanya huyo mtu akose furaha ndiyo anakiondoa kwanza ili USIJUTIE wokovu aliyokupa; Akiona unaendelea na wokovu anaondoa kimoja baada ya kingine kile ambacho kitakuondolea furaha ya wokovu wako mpaka vyote viishe na ndipo unafika mahali pa kuelea katika Utukufu wake.

Ukifika mahali ukakutana naye utasema NIMEMUONA MWANAUME, Yesu akitokeza katika maisha yako kila kitu kilichopinda kinakaa katika mstari wake; Maana mkononi mwake mnamema ya milele.

Huwezi kufikia toba ya kweli kama hujakutana na mwokozi wako, mtu aliyeokoka akisikia Neno linahubiriwa iwe lina muhusu au halimuhusu hasemi hili si la kwangu ni la fulani, bali ANAJITATHMINI mwenyewe na kuona kuwa AMEKOSEA ANAJIREKEBISHA au kama yuko sawa anamshukuru Mungu. Mtu aliyekombolewa huwa ANAJITENGENEZA ili azidi kuwa bora, lakini wale ambao hawajakombolewa pindi anaposikia Neno anasema hili siyo langu bali ni lafulani, kama wewe ni mmoja wao jua kuwa hujakombolewa bado, jitahidi ili ufikie katika TOBA YA KWELI. Mtu aliyekutana na Yesu huwa anasema ya kwake na Mungu wake na si ya watu wengine.

Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani. Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri,” 
Daudi alikuwa hasemi ya wenzake bali alikuwa anasema ya kwake ili apate KUKOMBOLEWA, Mungu anapendezwa na KWELI ya mtu iliyo MOYONI mwake.

Laana ikikushambulia, Unaishi kwa mashaka na hata kufa unakufa kabla ya wakati wako kufika. SIYO RATIBA ya Mungu wewe ufe mapema, bali Ratiba yake ni wewe UISHI mpaka muda ule aliokusudia YEYE ufike; Sio RATIBA YA MUNGU wewe Uishi kwa MASHAKA au DHIKI, Ratiba yake ni wewe uishi kwa KUCHANUA hapa chini ya jua.

Zaburi 109:14-16 “Uovu wa baba zake ukumbukwe mbele za BWANA, Na dhambi ya mamaye isifutwe. Ziwe mbele za BWANA daima, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. Kwa kuwa hakukumbuka kutenda fadhili, Bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, Hata akamfisha mtu aliyevunjika moyo,”

Baba yako akifanya dhambi ASIPOTUBU inakumbukwa kwako na unadaiwa, kila wakati ibilisi ANAKUSHITAKI kwa Baba wa Mbinguni na anakushinda. Hata UNAPOOMBA mbele za Mungu hakuna KINACHOTOKEA kwako, unafunga usiku na mchana na hakuna kinachotokea.

Zaburi 109:6-8“Uweke mtu mkorofi juu yake, Mshitaki asimame mkono wake wa kuume. Katika kuhukumiwa ataonekana hana haki, Na sala yake itadhaniwa kuwa ni dhambi. Siku zake na ziwe chache, Usimamizi wake na atwae mtu mwingine.”

Utajuaje Mkono wa Mungu uko juu yako? Utaona kila kitu au mtu anayeinuka kinyume chako ANASHINDWA. Zaburi 89:20-23 “Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu. Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu. Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa.” BWANA akikupaka mafuta anakutia NGUVU na FADHILI zake zinakuzunguka na yule anayekuonea ANAONDOLEWA kwako.

OMBI: Ee BWANA kama liko jambo lolote linalonikandamiza au kunirudisha nyuma naomba uliondoe leo katika maisha yangu.

 

Comments

comments

Comments are closed.